FCC KUADHIMISHA SIKU YA KIMATAIFA YA HAKI ZA MLAJI KWA KUTOA ELIMU KWA UMMA







Na Lilian Ekonga……

Tume ya Ushindani (FCC) inatarajia kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Haki za Mlaji Duniani kwa kutoa elimu kwa wadau na wananchi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uelewa kuhusu haki na wajibu wa walaji pamoja na wafanyabiashara.


Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Khadija Ngasongwa, alisema maadhimisho ya mwaka 2026 yanaongozwa na kaulimbiu isemayo “Safe Products, Confident Consumer” yaani “Bidhaa Salama, Imani kwa Mlaji.”


Alisema kaulimbiu hiyo inalenga kusisitiza umuhimu wa kuhakikisha kuwa bidhaa na huduma zinazotolewa sokoni ni salama, zinakidhi viwango vinavyokubalika kitaifa na kimataifa, na hazihatarishi afya, usalama wala maslahi ya walaji.


“Kaulimbiu hii pia inalenga kujenga imani ya walaji katika soko kwa kuhimiza uwazi, ubora na uwajibikaji kwa wafanyabiashara,” alisema Ngasongwa.


Aliongeza kuwa mlaji anayezingatia ubora huchangia ukuaji wa uchumi imara kwa kuchagua bidhaa na huduma zenye viwango stahiki. Aidha, wafanyabiashara wanaozalisha na kusambaza bidhaa bora hunufaika na ushindani wa haki, jambo linalochochea ubunifu, ufanisi na hatimaye kukuza uchumi wa taifa.





Akizungumzia mchango wa taasisi za kimataifa, Ngasongwa alisema kupitia kaulimbiu hiyo, Consumer International imeweka msisitizo mkubwa katika usalama wa bidhaa kwenye biashara mtandao.


Alisema biashara mtandao imeonekana kuwa na viatarishi vingi kwa walaji, ikiwemo ukosefu wa uwazi na uwajibikaji, pamoja na uwezekano wa bidhaa kutokidhi viwango vya ubora au kutowafikia walaji kama ilivyoelezwa.


Aidha, alibainisha kuwa Desemba 16, 2025, Shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo (UNCTAD) lilipitisha Kanuni Mpya za Usalama wa Bidhaa kwa Walaji (New Global Consumer Product Safety Principles) zinazolenga kuimarisha ulinzi wa walaji katika masoko ya kawaida na ya mtandao.





“Kanuni hizi zimepitishwa wakati ambapo takribani asilimia 44 ya nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa hazina mifumo madhubuti ya kisheria na kitaasisi ya kuhakikisha usalama wa bidhaa kwa walaji,” alisema.


Kwa upande wa FCC, alisema Tume hiyo kwa kushirikiana na wadau imeanzisha mchakato wa kutangaza viwango vya kitaifa kwa mujibu wa Sheria ya Ushindani Na. 8 ya mwaka 2003, kama ilivyorekebishwa, pamoja na kufanya utafiti wa soko la biashara mtandao nchini.


Alisema utafiti huo utasaidia katika kufanya maamuzi ya kisera yatakayolenga kuimarisha ulinzi wa walaji na watoa huduma wa biashara mtandao nchini.


Ngasongwa alisisitiza kuwa kama Mdhibiti wa Ushindani na Mlinzi wa Mlaji, FCC itaendesha maadhimisho hayo kwa kutoa elimu kuhusu haki na wajibu wa walaji.


“Lengo ni kuwajengea uwezo walaji kufanya maamuzi sahihi sokoni na kuchukua hatua pale kunapokuwa na ukiukwaji wa sheria. Matokeo yake, mlaji anakuwa katika nafasi nzuri ya kuisaidia Serikali katika juhudi za kudhibiti soko,” alisema.


Katika maadhimisho ya mwaka 2026, FCC itatoa elimu kupitia vipindi vya televisheni na redio za kitaifa na kijamii, mihadhara katika vyuo mbalimbali, pamoja na Kliniki za Walaji zitakazofanyika katika mikoa ya Pwani, Dodoma, Musoma, Njombe na Tanga.


Pia kutakuwa na semina kwa wafanyabiashara na taasisi zinazotumia mikataba ya walaji (Standard Form Consumer Contracts) tarehe 10 Machi 2026 katika ofisi za Dar es Salaam, pamoja na semina kwa wadau wa sekta ya ujenzi tarehe 11 Machi 2026 jijini humo. Elimu kwa umma pia itatolewa kupitia magari yanayotangaza (road shows).


“Nitumie fursa hii kuwakaribisha wananchi wenye changamoto zozote kuhusiana na bidhaa au huduma kusikiliza vyombo vya habari na kuhudhuria kliniki za walaji tulizoandaa mahsusi kupokea hoja, malalamiko na changamoto zao ili zipatiwe ufafanuzi na majawabu stahiki,” alisisitiza Ngasongwa.


Previous Post Next Post