DC ILALA AAHIDI USHIRIKIANO NA FCC KUDHIBITI BIDHAA BANDIA NA VIWANDA BUBU DAR







Na Lilian Ekonga, Dar es salaam

 Mapambano dhidi ya bidhaa bandia na viwanda bubu jijini Dar es Salaam yamepata nguvu mpya baada ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, kuahidi ushirikiano wa karibu kati ya ofisi yake na Tume ya Ushindani (FCC) ili kukomesha vitendo hivyo vinavyoathiri uchumi na usalama wa watumiaji.


Ahadi hiyo imetolewa wakati wa semina maalum ya wahariri wa vyombo vya habari iliyoandaliwa na FCC Februari 23 jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kuimarisha uelewa wa sera za ushindani, ulinzi wa mlaji na udhibiti wa masoko.


Akizungumza katika semina hiyo, Mpogolo alisema halmashauri zote za Jiji la Dar es Salaam zitaimarisha udhibiti na ufuatiliaji ili kuwabaini na kuwachukulia hatua kali wote wanaojihusisha na uzalishaji na usambazaji wa bidhaa zisizo halali, wakiwemo wamiliki wa viwanda visivyosajiliwa.


Alibainisha kuwa kumekuwepo na ongezeko la viwanda bubu vinavyozalisha bidhaa feki, hali inayochangia kuvuruga ushindani wa soko, kupunguza mapato ya Serikali na kuhatarisha afya pamoja na usalama wa wananchi. 




Alieleza kuwa kuimarishwa kwa nguvu kazi kutasaidia kudhibiti bidhaa zinazoingia nchini kabla hazijasambazwa sokoni, na hivyo kulinda soko la ndani pamoja na watumiaji.


Katika hatua nyingine, Mpogolo alieleza kuwa ushirikiano kati ya FCC na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) umeonyesha mafanikio makubwa, hususan katika kupunguza uingizwaji na usambazaji wa bidhaa bandia za kielektroniki, ikiwemo televisheni zilizokuwa zikiuzwa kwa wingi katika maeneo ya Kariakoo.



Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC), Khadija Ngasongwa, alisema taasisi hiyo inaendelea kutekeleza maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kufanya maboresho mbalimbali yanayolenga kufungua milango zaidi kwa wawekezaji na kuimarisha mazingira ya ushindani nchini.


Ngasongwa alisema FCC imejipanga kuhakikisha sheria ya ushindani inakuwa chachu ya kuvutia uwekezaji, kwa kuwa ni moja ya vigezo muhimu ambavyo wawekezaji huzingatia kabla ya kuwekeza katika nchi yoyote.





“Sheria yetu ya ushindani ni moja ya mambo ambayo mwekezaji hujiuliza anapokuja kuwekeza Tanzania. Anaangalia kama akizalisha bidhaa au kutoa huduma, je soko linalindwaje? Je, ushindani ni wa haki? Haya yote humsaidia kufanya maamuzi sahihi ya uwekezaji,” alisema Ngasongwa.


Alifafanua kuwa namna soko linavyoendeshwa na kusimamiwa kwa misingi ya ushindani wa haki ndiyo humvutia mwekezaji, kwani humwezesha kufanya tathmini na makadirio (prediction) ya faida na ukuaji wa biashara yake kwa uhakika zaidi.


Aidha, alisema FCC imekuwa ikifanya tafiti mbalimbali za masoko ili kuongeza ufanisi wa usimamizi na kutoa takwimu zitakazosaidia wafanyabiashara na wawekezaji kufanya maamuzi sahihi.




Ngasongwa alibainisha kuwa maboresho hayo yanaenda sambamba na mifumo ya kisasa ya kiutendaji iliyoanza kutumika tangu Desemba mwaka jana, kwa lengo la kurahisisha utoaji wa huduma na kuongeza uwazi katika utekelezaji wa majukumu ya tume.




 






Previous Post Next Post