Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), CPA Profesa Sylvia Temu, amewataka wahasibu na wakaguzi wa hesabu nchini kuzingatia misingi ya uaminifu na uadilifu katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku, ili kuzuia upotevu wa mapato ya Serikali na kuchochea maendeleo ya taifa.
Akizungumza katika mahafali ya 48 ya NBAA yaliyofanyika tarehe 28 /03 / 2025 katika Kituo cha Mikutano cha APC jijini Dar es Salaam, Profesa Temu alisema taaluma ya uhasibu inahitaji watu wenye maadili thabiti na wanaozingatia ukweli katika kazi zao.
Mahafali hayo yaliwahusisha wahitimu 531 kutoka fani mbalimbali za uhasibu na ukaguzi wa hesabu, hatua ambayo imeelezwa kuwa ni mchango mkubwa katika kuongeza wataalamu wenye sifa nchini.
“Ni muhimu mkafanya kazi kwa weledi mkubwa, mkizingatia sheria, kanuni na taratibu za taaluma yenu. Epukeni rushwa na ushawishi unaoweza kuchafua tasnia hii,” alisema Profesa Temu.
Alisisitiza zaidi kuhusu maadili kwa kusema, “Tafadhali endeni msijichafue na msituchafue, msiichafie taaluma. Muwe watu wenye maadili mema na wanaoaminika kwa kuwa mnasimamia tasnia ya namba, na namba hazidanganyi.”
Aidha, aliwahimiza wahitimu hao kuendelea kujiongezea ujuzi kwa kujifunza mbinu mpya na kuendana na kasi ya maendeleo ya teknolojia duniani, ili waweze kushindana katika soko la ajira la kimataifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA Pius Maneno, alisema uamuzi wa kuanza kufanya mahafali mwezi Machi umetokana na maoni ya wadau, lengo likiwa ni kuwasaidia wahitimu kuingia mapema kwenye soko la ajira bila kuchelewa.
Alieleza kuwa wahitimu hao walifaulu mitihani ya Novemba 2025 na Februari 2026, wakijumuisha wahitimu 49 wa cheti cha uandishi wa vitabu vya hesabu, 399 wa shahada ya juu ya uhasibu, 9 wa ulinganifu wa shahada hiyo, 53 wa stashahada ya viwango vya kimataifa vya hesabu, 18 wa stashahada ya ukaguzi wa ndani, na 3 wa astashahada ya viwango vya kimataifa vya hesabu.
Hatua hiyo inaonesha juhudi za NBAA katika kukuza taaluma ya uhasibu na kuhakikisha nchi inapata wataalamu wenye uwezo, uadilifu na ushindani wa kimataifa.



