Na Lilian Ekonga ……Dar es Salaam
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) imeridhishwa na utekelezaji wa miradi wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), baada ya kutembelea na kukagua majengo ya makazi yaliyojengwa cadanian Masaki jijini Dar es Salaam.
Akizungumza mara baada ya ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Masanja Kadogosa, amesema majengo hayo yanaonesha thamani halisi ya fedha iliyowekezwa, huku akibainisha kuwa kila jengo linakadiriwa kugharimu takribani shilingi bilioni 4.6 na lina uwezo wa kuhudumia familia 12 kwa kila jengo
Kadogosa amesema kamati imejiridhisha kuwa miradi hiyo ni sehemu muhimu ya utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), hususan katika kuhakikisha upatikanaji wa makazi bora kwa wananchi, hasa katika miji mikubwa kama Dar es Salaam.
Ameipongeza TBA kwa ubunifu wa mifumo ya utekelezaji wa miradi, ikiwemo matumizi ya modeli inayowezesha ujenzi kufanyika kwa ufanisi hata kwa kutumia mikopo, hatua inayosaidia kupunguza utegemezi wa fedha za serikali.
Kwa upande wake, kamati hiyo imeitaka TBA kuendelea na awamu nyingine ya miradi inayotarajiwa kuanza mwaka ujao wa fedha, ili kuongeza upatikanaji wa nyumba na kukidhi mahitaji yanayoongezeka.
Akitoa ufafanuzi wa mpango huo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Charles Msonde, amesema serikali kupiti Wakal wa majengo (TBA) imeweka mkakati wa kujenga zaidi ya majengo 18 katika eneo hilo.
Amesema majengo matatu tayari yamekamilika, kila moja likiwa na uwezo wa kuhudumia familia 12, hivyo kufikia jumla ya familia 36, na kwamba yote tayari yamepangiwa wakazi.
Msonde ameeleza kuwa mafanikio hayo yametokana na matumizi ya mapato ya ndani ya TBA, hatua inayopunguza utegemezi wa bajeti ya serikali.
Aidha, amebainisha kuwa mabadiliko ya sheria ya wakala ya mwaka 2003 yameiwezesha TBA kutumia mfumo wa ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP) ili kuongeza kasi ya ujenzi wa makazi bora nchini.




