Na mwandishi wetu, Dar es salaam
Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) CPA. Prof. Sylvia Temu ameongoza viongozi na watumishi wa bodi hiyo kumkaribisha rasmi na kumkabidhi ofisi Mkurugenzi Mtendaji mpya CPA. Prof. Siasa Mzenzi na kuahidi kumpa ushirikiano wa dhati ili kuhakikisha bodi hiyo inaendelea kuimarisha taaluma muhimu ya uhasibu na ukaguzi Nchini.
Akizungumza wakati wa kukaribishwa kwake, katika makao makuu ya ofisi za bodi hiyo jijini Dar es Salaam, Prof. Siasa Mzenzi ameahidi kuendeleza ushirikiano na wadau wote wa uhasibu na ukaguzi nchini, ili kuhakikisha tasnia hiyo inaendelea kuongeza thamani na mchango wake katika maendeleo ya uchumi wa Taifa.
Prof. Siasa Mzenzi anachukua nafasi hiyo kufuatia kustaafu kwa Mkurugenzi Mtendaji, CPA. Pius Maneno, ambaye amestaafu rasmi utumishi wa umma Machi 29, 2026, baada ya kutoa mchango mkubwa katika kuendeleza taaluma hiyo nchini.

