Mkurugenzi wa Ujenzi NHC Mhandisi Haikamen Mlekio (kulia) akimwongoza Bw. Jerry Silaa (katikati) na ujumbe wake kuelekea kwenye nyumba ya mfano
Mkurugenzi Mkuu wa NHC Bw. Hamad Abdallah akiwaeleza jambo wajumbe wa Kamati hiyo kuhusiana na nyumba hizo.
Meneja wa mradi wa Iyumbu Msanifu Majengo Frank Mambo akimkaribisha Mwenyekiti wa Bodi Dkt. Sophia Kongela eneo la tukio.
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma - PIC imelipongeza Shirika la nyumba la Taifa kwa kazi nzuri inayofanya katika kuendeleza miji na kujenga makazi bora kwa wananchi.
Hayo yamesemwa leo na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mheshimiwa Jerry Silaa wakati wa ziara ya Kamati hiyo katika nyumba za makazi Iyumbu kwenye mradi unaotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa - NHC.
Mheshimiwa Silaa amesema kuwa baada ya kutembelea mradi huo Kamati yake imeridhishwa na hatua iliyofikiwa na kuitaka NHC kuendelea kujenga nyumba za namna hiyo katika maeneo mengine nchini ili kuweza kuisaidia Serikali katika azma yake ya kuongeza makazi bora kwa wananchi.
“Kamati inalipongeza sana Shirika kwa hatua nzuri iliyofikiwa ya utekelezaji wa mradi huu ambao umechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza adha ya makazi kwa watumishi mbalimbali mara baada ya makao makuu ya Serikali kuhamia Dodoma, hii ni kuonesha kuwa NHC inatambua wajibu iliyo nao kwa nchi na watu wake katika kuhakikisha inawapatia makazi bora watu wake” Alisema Silaa
Amebainisha kuwa Shirika la Nyumba la Taifa pamoja na mipngo na mikakati iliyo nayo kwa nchi lakini pia limekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha inabadilisha baadhi ya miji kwa kujenga majengo makubwa ya biashara na nyumba za makazi na kwamba kwa kufanya hivyo inaonesha dhahiri kuwa NHC inaunga mkono juhudi za Serikali.
Wakichangia taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa NHC Bw. Hamad Abdallah juu ya utekelezaji wa mradi wa nyumba 1000 Jijini Dodoma, Wajumbe wa Kamati hiyo walilipongeza Shirika la Nyumba la Taifa kwa kazi nzuri inazofanya. Wabunge walitaka kujuwa namna Shirika linavyosaidia ujenzi wa nyumba za gharama nafuu na kama uwekezaji unaofanyika Dodoma unaweza kuenezwa katika mikoa mingine.
Pia Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurungenzi Dkt. Sophia Kongela alianza kwa kuwashukuru wajumbe wa Kamati kwa kuwa imekuwa ikiisimamia vyema NHC na kuahidi kuyafanyia kazi maagizo matano yaliyotolewa na Kamati hiyo kwa ajili ya kuleta tija kwa Shirika na Taifa. Alieleza kuwa Shirika linatekeleza miradi 12 ya uwekezaji ukiwemo mradi wa Samia Housing Scheme ambao utajengwa nyumba 5000 kwa gharama ya shilingi 466 bilioni.
Aidha, Dkt. Kongela kwa niaba ya Bodi ya Wakurugenzi ya NHC ameialika kamati hiyo kutembelea miradi mingine mbalimbali inayotekelezwa na Shirika jijini Dar es Salaam ukiwemo mradi wa Morocco Square.
Aidha, Mkurugenzi Mkuu wa NHC Bw. Hamad Abdallah akiuelezea mradi huo alisema kuwa Shirika linatarajia kupata faida ya shilingi Bilioni 3.8 kutokana na mradi wa Iyumbu na kwamba mradi huo umeweza kuzalisha ajira mbalimbali zikiwemo za Wahandisi, mafundi wa kawaidia, vibarua wa kawaida, baba na mama lishe watunza stoo.
Aidha amezungumzia mauzo katika mradi huo ambapo mpaka sasa nyumba 163 zimeuzwa ambazo ni sawa na asilimia 54% ambapo kati ya hizo nyumba 108 zimeshalipiwa na nyumba 55 ziko kwenye hatua mbalimbali za malipo.
Pamoja na faida iliyotarajiwa kupatikana Bw. Abdallah amezungumzia pia changamoto mbalimbali walizokabiliana nazo katika kutekeleza mradi huo.
“Kupanda kwa gharama ya vifaa vya ujenzi husani chuma wakati wa kipindi cha UVIKO 19 na vita ya Ukraine na Urusi kumesababisha mradi huu kutokamilika kwa wakati ambapo tulitarajia kuukamilisha katika kipindi cha miezi 18” Alisema Bw. Abdallah.
Mkurugenzi Mkuu amebainisha changamoto nyingine kuwa ni baadhi ya wauzaji wa vifaa kutokuwa na uwezo wa kuuza vitu vingi zaidi kwa wakati mmoja.
Hata hivyo Bw. Abdallah amesema kuwa Shirika liko mbioni kukamilisha mradi huo kwani kazi zilizobaki ni chache.
Kabla ya kuhitimisha kikao hicho Mwenyekiti wa PIC alitoa maagizo ya Kamati kwa Shirika ambayo ni kuhakikisha NHC inakuwa na mpango madhubuti wa mauzo na masoko (pre sale), kuhakikishia NHC inapitia upya mpango wa mauzo kwenye mradi hasa kipengele cha kulipia 10% kama malipo ya awali kwa watumishi wa umma na kuhakikisha NHC inaweka mpango mkakati kuratibu upatikanaji wa miundombinu kama vile barabara, maji na umeme kabla ya kuanza kwa mradi husika.
Maazimio mengine ni kuhakikisha NHC inafanya utafiti wa soko la nyumba katika mikoa mbalimbali ili kuongeza wigo wa huduma inazotoa hatua itakayosaidia kuhudumia wananchi wengi zaidi na kuongeza mapato kwa Shirika.