Na Lilian Ekonga DAR ES SALAAM,
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema jukumu la Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) ni kuandaa na kusambaza vitabu vya shule, vikiwemo vya kiada na ziada, kwa kushirikiana na waandishi wa ndani ili kuhakikisha wanafunzi wanapata machapisho bora.
Amesema pamoja na kuandaa vitabu hivyo, ipo haja kubwa ya kuibua na kulea waandishi bunifu wa Kitanzania ili kuongeza upatikanaji wa vitabu vyenye ubora vinavyoweza kutumika shuleni na wakati huohuo kuimarisha fasihi ya Kiswahili.
Prof. Mkenda aliyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa vitabu vya washindi wa Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu, akieleza kuwa lengo la tuzo hiyo ni kuongeza idadi ya vitabu vinavyoandikwa na Watanzania na kuhamasisha uandishi wa kibunifu.
Alifafanua kuwa tuzo hiyo imepewa jina la Julius Kambarage Nyerere kwa kutambua mchango wake mkubwa katika fasihi ya Kiswahili.
“Mwalimu Nyerere aliandika mashairi na kufasiri kazi za kifalsafa pamoja
na tamthilia za Shakespeare kwa vina na mizani sahihi, hivyo kuenzi urithi wake wa kiutamaduni na kielimu,” alisema Prof. Mkenda.
Akizungumzia changamoto zinazoikabili sekta ya uchapishaji, alisema Serikali imeweka mkakati wa kununua na kusambaza vitabu vya washindi wa tuzo hiyo shuleni na katika maktaba mbalimbali ili kuhakikisha soko la uhakika kwa wachapishaji na kuongeza kipato kwa waandishi. Kupitia mpango huo, aliongeza, uandishi utapata thamani ya kiuchumi na kijamii huku sekta ya uchapishaji ikipewa fursa ya kukua.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa watoto wa Kitanzania kusoma vitabu vya ndani, akieleza kuwa kutegemea vitabu vya nje pekee hakutoshi katika kujenga utambulisho wa kitaifa. Alisema vitabu vinavyoakisi mazingira, historia na tamaduni za Tanzania huwasaidia watoto kujitambua na kuthamini urithi wao.
Aliongeza kuwa uzinduzi wa vitabu vya washindi wa tuzo hiyo ni hatua muhimu katika kuhifadhi utamaduni, kuimarisha elimu na kuandaa vizazi vijavyo, na ni sehemu ya mkakati mpana wa Serikali wa kuwekeza katika elimu, fasihi na kukuza sekta ya uchapishaji nchini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dkt. Aneth Komba, alisema Serikali imetenga shilingi bilioni moja kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kwa ajili ya Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu.
Amesema kati ya fedha hizo, shilingi milioni 400 zimetumika kuchapa na kusambaza vitabu vya washindi wa kwanza katika kila fani, hatua iliyowezesha kuchapishwa kwa jumla ya nakala 142,000 zitakazogawiwa katika shule zote nchini kwa wastani wa vitabu nane hadi kumi kwa kila shule.
Dkt. Komba amesema uzinduzi huo unakamilisha zawadi ya nne kwa washindi baada ya kupokea vyeti na fedha taslimu, huku kazi zao sasa zikichapishwa na kusambazwa rasmi katika shule na maktaba ili kuwafikia wanafunzi na jamii kwa ujumla.
Aidha, amesema vitabu hivyo tayari vimepata ithibati ya Kamishna wa Elimu, hatua inayoruhusu vitumike rasmi kama nyenzo za kufundishia na kujifunzia shuleni.
Vitabu vilivyozinduliwa ni vya fani tatu za fasihi ambazo ni riwaya, ushairi na hadithi za watoto. Riwaya inaitwa Garasa, diwani ya ushairi Ngoma ya Muwele na kitabu cha hadithi za watoto Maziwa ya Kuku.
The people



