Na Lilian Ekonga, Dar es salaam
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama hususan Jeshi la Polisi, imefanya operesheni maalum katika vijiji vya Marieni na Mhero, kata ya Chome, wilaya ya Same, Kilimanjaro kuanzia tarehe 10 hadi 16 Februari 2026.
Operesheni hiyo imefanikiwa kukamata kilogramu 299.8 za dawa za kulevya aina ya mirungi na kuteketeza ekari 203 za mashamba ya mirungi. Watu saba wamekamatwa kuhusiana na uhalifu huo.
Akizungumza mara baada ya operesheni, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, alisema licha ya jitihada za muda mrefu za utoaji elimu na operesheni za mara kwa mara, bado kuna baadhi ya watu wanaoendelea kukaidi sheria.
“Serikali imefikisha huduma muhimu ikiwemo umeme na maji safi, pamoja na miradi ya kilimo na ufugaji. Wananchi wengi wameanza kujishughulisha na mazao mbadala kama vile vitunguu, viazi, kabeji, parachichi na kahawa,” alisema Kamishna Jenerali Lyimo.
Aidha, alisisitiza kuwa DCEA itaendelea kushirikiana na viongozi wa vijiji, kata, wilaya na mkoa pamoja na wadau wengine kutoa elimu na kutekeleza operesheni endelevu ili kuhakikisha tatizo la mirungi linadhibitiwa kikamilifu katika mkoa wa Kilimanjaro.
Kwa upande wake, Mtendaji wa Kijiji cha Mhero, Hamad Waziri Hamad, alisema operesheni hiyo itasaidia vijana kuachana na kilimo na matumizi ya mirungi, kwani kilimo hicho kilikuwa na madhara makubwa, ikiwemo vitendo vya uhalifu na kuhatarisha usalama wa wakazi.
Wakazi wa Chome, wakiwemo Rafael Kisenge, mkulima wa mazao mseto, walisema uwepo wa fursa za kilimo halali ni mkubwa kutokana na ardhi yenye rutuba na ruzuku ya pembejeo. Kisenge alisema, “Hatujahitaji tena kilimo haramu. Hata katika eneo dogo tunapata faida.”
Aidha, Mohamed Athuman Mbwabomkazi, dereva wa maroli, alisema baadhi ya wakazi waliokuwa wakilima mirungi wameshaachana na kilimo haramu, huku wachache waliodhani kuendelea, wakishikiliwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.
DCEA inawaomba wananchi kushirikiana katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwa maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.





