Na Mwandishi Wetu,
Naibu Waziri wa Uchukuzi Atupele Mwakibete amelitaka Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuhakikisha linakamilisha ujenzi wa Miundombinu ya Reli ndani ya Bandari ya Tanga ili kurahisisha utoaji wa mizigo bandarini hapo.
Naibu Waziri Mwakibete ametoa maagizo hayo Mkoani Tanga mara baaada ya kukagua maendeleo ya mradi wa upanuzi wa gati katika bandari ya Tanga na kugundua kusua sua kwa uboreshaji wa miundombinu ya reli na kusema kuwa uwepo wa reli bandarini hapo utaifanya bandari kuwa na ufanisi kwani mzigo utatumia muda mfupi kukaa bandarini na hivyo kupunguza gharama kwa wafanyabiashara.
“Ufanisi wa Bandari unategemea wepesi na uharaka wa kushusha na kupakia mizigo inayoletwa na meli na kwa hapa reli ni ya muhimu sana lakini TRC hamuonekani kama mnakwenda na kasi ya maboresho mnayoyaona yanafanyikaa bandarini hapa, niwahakikshie nimekuja leo hapa nitarudi tena ndani ya siku chache kuja kuona mmefikia mmefikia wapi kwenye utekelezaji wa maelekezo yangu’ amesema Naibu Waziri Mwakibete.
Naibu Waziri Mwakibete ameipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari kwa kufikisha asilimia zaidi ya 98 ya utekelezaji wa mradi wa maboresho ya gati na kuanza kulitumia gati kwani kuanza kuhudumia meli bila kutumia matishali kutaongeza ufanisi na tija na kuongeza pato la Mamlaka.
Aidha, Naibu Waziri Mwakibete ameitaka TPA kuhakikisha inatenga eneo kwa ajili vyombo vidogo vidogo kama majahazi na mitumbwi ili kupunguza changamoto za kuwa na bandari bubu kwa sababu ya kukosa maeneo rasmi ya kufanyia shughuli zao.
Naye Mhandisi wa Miradi kutoka TPA, Hamisi Mbutu amesema kukamilika kwa Ujenzi wa gati mbili bandarini hapo kumeonyesha matokeo chanya kwani meli kubwa za shehena mbalimbali zimeanza kuitumia bandari hiyo hali itakayopunguza mlundikano wa mizigo katika bandari ya Dar es Salaam.
Kwa Upande wake Mkuu wa Kitengo cha Mipango na Uwekezaji kutoka Bandari ya Tanga, Tumgonze Kabigumila amesema Mamlaka inajipanga kuendelea kutafuta masoko ili kuweza kuhudumia shehena nyingi kwa muda mchache.
Kabigumila ameongeza kuwa ndani ya mwezi mmoja baada ya kutumia gati hizo mpya tayari mzigo wa tani zaidi ya laki moja na elfu thelathini imehudumia .
Mradi wa uboreshaji wa bandari ya Tanga ni moja ya mikakati inayotekelezwa na TPA kuhakikisha kuwa mizigo inahudumiwa katika bandari zote badala ya kuhudumiwa kwa wingo katika bandari ya Dar es Salaam.