CHADEMA YAUNGANA NA WADAU WA HABARI KUPIGANIA MABADILIKO YA SHERIA YA HABARI NCHINI


Na Mwandishi Wetu

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeeleza kupigania mabadiliko ya Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 wakati wa mazungumzo yake na Chama cha Mapindizi (CCM) ili vyombo vya habari nchini viwe huru kuripoti mikutano ya Kisiasa ya hadhara. 


Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano, Uenezi na Mambo ya Nje wa CHADEMA, John Mrema amebainisha hayo Jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa ya uzinduzi wa mikutano ya hadhara ya Chama hicho utakaofanyika Jijini Mwanza Januari 21, 2023. 

Mrema amesema sheria iliyopo inafifisha uhuru wa vyombo vya habari katika kutekeleza majukumu yao hasa katika kipindi hiki ambacho mikutano ya hadhara imeruhusiwa, jambo ambalo litawanyima fursa ya kutekeleza majukumu yao.

 “Kwenye mazungumzo yanayoendelea, kati ya sheria ambazo tunafikiri ni sheria za awali za kufanyiwa marekebisho au kuandikwa upya, ni pamoja na Sheria ya Huduma za Habari kwa sababu huwezi kurudi kwenye mikutano kama umevifunga vyombo vya habari mikono nyuma, Mikutano hiyo haitawafikia wananchi" amesema Mrema.

 Mbali na Chadema, wadau wengi wakiongozwa na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) wamekuwa wakipigania mabadiliko ya sheria hiyo ili kuviwezesha vyombo vya habari na wadau wengine wakiwemo wananchi kuongozwa na sheria bora.

Previous Post Next Post