NSSF yaweka rikodi ya mafanikio katika ukuaji wa Mfuko



Na  MWANDISHI WETU

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Masha Mshomba,  amesema Mfuko umepata mafanikio makubwa na umekuwa kwa kasi sana.

Mshomba alisema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akitoa Taarifa ya Utendaji wa  Mfuko pamoja na Vipaumbele vya Mfuko kwa mwaka wa Fedha  2022/23.

"Tumepata mafanikio makubwa katika suala zima la ukuaji wa Mfuko na hii imesababishwa na sababu kadhaa ikiwemo kuweka misingi imara na madhubuti ya ukusanyaji wa mapato," alisema.

Mshomba alisema ukuaji huo ni mkubwa tofauti na miaka miwili ya nyuma iliyopita ambapo thamani ya Mfuko ilikuwa ni Shilingi Trilioni 4.3 na kuwa ukuaji huo umechangiwa na ongezeko la makusanyo ya michango.

Alisema katika mwaka wa fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022, Mfuko ulikusanya zaidi ya Shilingi Trilioni 1.42 kwamba makusanyo hayo ni zaidi ya hata bajeti ambayo walijipangia iliyokuwa Shilingi Trilioni 1.38.

Mshomba alisema pia Mfuko umeboreshaji sana udhibiti wa matumizi jambo ambalo limechangia ukuaji wa NSSF.

Mafanikio mengine yaliyopatikana, alisema ni uboreshaji wa huduma hasa kwa kutumia mifumo mbalimai ya TEHAMA ambapo sasa mwanachama na wadau wanaweza kupata huduma popote walipo bila ya kufika katika ofisi za NSSF kwa kutumia mifumo ya waajiri na wanachama yaani Employer Potal na Member Potal.

Mshomba alisema Mfuko pia unapata matokeo mazuri sana katika Uwekezaji hasa ukizingatia kuwa wanawekeza katika maeneo salama ambapo katika kipindi cha miaka miwili uwekezaji umeleta mapato makubwa.

"Ilikuwa haijafikiwa NSSF kuweza kupata mapato ya mwaka zaidi ya Shilingi bilioni 500 lakini katika mwaka huu wa fedha umepata zaidi ya Shilingi bilioni 600," alisema.

Alisema matokeo hayo ya uwekezaji yametokana na Mfuko kujikita zaidi katika uwekezaji kwenye maeneo ambayo yanaleta faida kwa Mfuko na kuhakikisha wanaudhibiti wa fedha.

Mshomba alisema chachu kubwa ya mafanikio ya NSSF imechagizwa na kasi ya utendaji wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa sababu amekuwa chachu ya ongezeko kubwa la wawekezaji hapa nchini.  
Previous Post Next Post