Na Lilian Ekonga Dar es salaam
Serikali imeahidi kuendelea kulinda uwekezaji katika sekta ya usafiri wa majini, ikiwemo meli, boti na vyombo vingine vya majini, huku ikilitaka Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kuimarisha usimamizi wa sekta hiyo na kuweka mikakati ya kuongeza idadi ya wataalamu wa kutosha.
Akizungumza baada ya kutembelea Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (SABASABA), Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, amesema Serikali imejipanga kuhakikisha wawekezaji katika sekta ya usafiri wa majini wanafanya shughuli zao katika mazingira salama na yenye uhakika.
Amesema ulinzi wa raia, wasiokuwa raia pamoja na mali zao ni miongoni mwa vipaumbele vya Serikali kupitia taasisi zake, hatua inayolenga kuongeza imani ya wawekezaji na kuvutia uwekezaji zaidi katika sekta ya uchumi wa buluu.
Kwa mujibu wa Kihenzile, uchumi wa buluu unaendelea kuwa nguzo muhimu katika kukuza uchumi wa Taifa, kuongeza fursa za ajira na kuchochea shughuli mbalimbali za biashara zinazohusiana na sekta ya usafiri wa majini.
Aidha, amesema ukuaji wa biashara katika bandari za Tanzania umeongeza kwa kasi mahitaji ya wataalamu wa sekta ya bahari, akieleza kuwa kiwango cha mizigo kilichotarajiwa kufikiwa mwaka 2030 kilifikia lengo hilo mapema mwaka 2022.
Amesema mafanikio hayo yametokana na uongozi madhubuti, kuimarika kwa diplomasia ya uchumi pamoja na ushiriki mkubwa wa sekta binafsi katika shughuli za kiuchumi.
Kihenzile amesema ongezeko la shughuli na mizigo katika bandari linahitaji kuongezwa kwa wataalamu mbalimbali wa sekta ya bahari, wakiwemo manahodha, wasaidizi wa mabaharia na wataalamu wengine watakaokidhi mahitaji ya sekta hiyo inayokua kwa kasi.
Kutokana na hali hiyo, amelitaka TASAC kutotekeleza jukumu lake la udhibiti pekee, bali kushirikiana na Serikali na wadau wengine kuweka mikakati ya kuzalisha wataalamu wa kutosha ili kuendana na kasi ya ukuaji wa sekta ya usafiri wa majini.
Amesema hatua hiyo ni muhimu katika kuhakikisha Tanzania inakuwa na wataalamu wenye uwezo wa kuhudumia sekta ya bahari na kutumia kikamilifu fursa zinazotokana na ukuaji wa uchumi wa buluu.
Habari lilina

