DKT. MSONDE AIPONGEZA TEMESA KWA MAGEUZI YA KIDIJITALI

 







Na Lilian Ekonga. Dodoma 



Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Dkt. Charles Msonde, ameupongeza  Wakala  wa  Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) kwa mageuzi makubwa ya kidijitali yaliyoboresha huduma za matengenezo ya magari ya Serikali na kuongeza uwazi, ufanisi pamoja na usalama wa watumiaji wa vyombo vya usafiri.


Dkt. Msonde ametoa pongezi hizo leo alipo tembelea  banda la TEMESA katika Maonesho ya 33 ya Kitaifa ya Kilimo (Nane Nane 2026) yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni, jujini Dodoma.


Amesema TEMESA ya sasa imebadilika kwa kiwango kikubwa tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma, ambapo mifumo ya kisasa imeondoa utegemezi wa makadirio ya kibinafsi katika matengenezo ya magari.



Alieleza kuwa mfumo wa kidijitali unaotumiwa na TEMESA unawezesha taarifa za gari kuonekana kwa wakati halisi, huku gharama za vipuri na matengenezo zikiamuliwa kwa viwango vinavyofanana nchini kote, jambo linaloongeza uwazi na kulinda matumizi sahihi ya fedha za umma.


Dkt. Msonde pia aliwapongeza mafundi wa TEMESA kwa kuendelea kuongeza umahiri wao, akisema huduma zinazotolewa sasa zina ubora unaoendana na viwango vya kitaalamu, huku magari yanayotengenezwa yakitolewa kwa dhamana (guarantee), hatua inayoongeza imani kwa wateja.


Aidha, alisema TEMESA ina jukumu muhimu la kulinda thamani ya fedha za Serikali kwa kuhakikisha matengenezo yanafanyika kwa viwango vinavyostahili na kuzuia upotevu wa rasilimali kupitia mifumo madhubuti ya usimamizi.


Alisisitiza kuwa ubora wa matengenezo ya magari na vivuko unachangia moja kwa moja usalama wa watumishi wa umma na wananchi, hivyo akautaka wakala huo kuendelea kuboresha huduma zake ili kuimarisha utoaji wa huduma za usafiri nchini.


Kwa upande wake, Meneja Masoko na Uhusiano kwa Umma- TEMESA, Bi. Martha Joachim, amesema miongoni mwa maboresho yaliyofanywa ni kuhuisha huduma ya ukodishaji wa mitambo kupitia Mfumo wa TIMIS, ambapo wateja sasa wanaweza kuwasilisha maombi ya ukodishaji kwa njia ya kidijitali, hatua iliyopunguza urasimu na muda wa kupata huduma.



Previous Post Next Post