WAKULIMA WA IRINGA WANUFAIKA NA MASOKO YA UHAKIKA KUPITIA IFCU






 Na mwandishi wetu


Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Iringa (IFCU) kimesema kinaendelea kuleta mageuzi katika sekta ya kilimo kwa kuwaunganisha wakulima na masoko ya uhakika, kusambaza pembejeo kwa wakati na kuhamasisha uzalishaji wa mazao yenye virutubisho, hatua inayochochea usalama wa chakula, kupunguza udumavu na kuongeza kipato cha wakulima.


Akizungumza katika Maonesho ya 31 ya Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, Meneja wa IFCU, Tumaini Lupora, alisema chama hicho kinashiriki maonesho hayo kwa mwaka wa tatu mfululizo kikionyesha mafanikio ya wakulima wake pamoja na bidhaa mbalimbali zinazozalishwa kupitia mfumo wa ushirika.


Alisema miongoni mwa bidhaa zinazovutia wananchi ni maharage yenye virutubisho vya madini ya chuma na zinki pamoja na unga wa mahindi ya njano wenye vitamini A, mazao ambayo yameanza kuzalishwa kwa lengo la kukabiliana na tatizo la udumavu na utapiamlo, hususan kwa watoto na makundi yenye uhitaji mkubwa wa lishe bora.


Lupora alisema IFCU kwa sasa inahudumia vyama vya msingi vya ushirika 63 vilivyopo katika wilaya za Iringa, Kilolo na Mufindi, vyenye wanachama zaidi ya 8,600 huku huduma zake zikifika kwa zaidi ya wakulima 50,000 kupitia usambazaji wa pembejeo, elimu ya kilimo bora, masoko na kuongeza thamani ya mazao.


Alieleza kuwa kupitia mfumo wa ushirika, wakulima wameondokana na changamoto ya kuuzwa mazao kwa vipimo visivyo rasmi, kwani kwa sasa mazao yote huuzwa kwa mizani inayotambulika, hali inayowawezesha kulipwa stahiki zao kulingana na uzito halisi wa mazao wanayouza.


Aidha alisema katika msimu wa kilimo wa 2025/2026, chama hicho kilikusanya zaidi ya kilo milioni 2.3 za mahindi na kuwalipa wakulima zaidi ya Shilingi bilioni 5.5, mafanikio yanayotokana na kuimarika kwa masoko na ushirikiano kati ya Serikali, vyama vya ushirika na wadau wa maendeleo.


Kwa upande wake, mkulima wa mahindi na maharage kutoka Halmashauri ya Mufindi, Paul Mwinuka, alisema ushirika umebadili maisha ya wakulima wengi kwa kuwawezesha kupata mbegu bora, mbolea za ruzuku na masoko ya uhakika, hatua iliyomsaidia kuongeza uzalishaji kutoka ekari chache hadi kulima maeneo makubwa zaidi na kuboresha kipato chake.



Mwinuka alisema kupitia ushirika wakulima hawana hofu ya kukosa soko, akibainisha kuwa mikataba inayofungwa na taasisi mbalimbali ikiwemo Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) imeongeza uhakika wa mauzo ya mahindi na kuwapa wakulima motisha ya kuongeza uzalishaji kila mwaka.


Naye Mratibu wa We Effect Tanzania, Frank Ademba, alisema taasisi hiyo inaendelea kushirikiana na IFCU katika kujenga uwezo wa vyama vya ushirika kupitia programu za kilimo endelevu, kilimo ikolojia, usawa wa kijinsia, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuongeza thamani ya mazao.


Alisema lengo la ushirikiano huo ni kuhakikisha wakulima wanazalisha mazao yenye tija na lishe, wanapata masoko yenye ushindani na kuongeza kipato, huku wakichangia kuimarisha usalama wa chakula nchini.



Lupora alisema katika mpango mkakati wa miaka mitano wa IFCU wa 2026 hadi 2030, chama hicho kinatarajia kuwafikia zaidi ya wakulima 100,000 kwa kuwapatia huduma za ushirika, elimu ya kilimo bora, pembejeo, masoko na teknolojia za kuongeza uzalishaji, ikiwa ni sehemu ya mchango wake katika kuifanya Tanzania kuwa taifa lenye usalama wa chakula na kilimo chenye tija.

Previous Post Next Post