MTANDAO wa kutokomeza Ndoa za Utotonini Nchini(TECMN) umesikitishwa na kauli iliyotolewa na Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro, kuwa serikali haitaibadilisha sheria ya ndoa ya mwaka 1971 mpaka ipate ridhaa ya taasisi za dini ili ibadlishe sheria hiyo.
Hivyo, Mtandao huo umesema kauli hiyo inapingana na maamuzi ya katiba kama ilivyoelezewa vyema kwenye ibara ya 107A ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na kuheshimu maamuzi yaliyotolewa na Mahakama kuu na mahakama ya Rufani ambazo ziliamua kwamba sheria ya ndoa katika kifungu cha 13 na 17 inakizana na katiba yetu na kuitoa maamuzi kuwa vifungu hivyo(13 na 17) vibadilishwe.
Akizungumza na waandishi wa habari mapema leo Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Msichana Intiative, Rebeca Gyumi, amesema wakati wote kunapokuwa na mgongano kati ya dini, mila na sheria, sheria ndio hutawala na kutumika.
Rebeca, amesema suala la umri wa kuolewa limetolewa uamuzi na mahakama kuwa umri ni miaka 18 .
"Hukuna maamuzi yeyote au taratibu nyingine au kigezo cha dini kinaweza kutengua maamuzi hayo" amesema Rebeca.
Kwa Upande wake, Wakili Getrude Dyabeno amesema kauli ya Waziri inakizana na hali halisi kwani nchi yetu haiongozwi na dini, ingawa watu wake wana dini mbalimbali, hivyo kujadili suala la Sheria ya Ndoa kwa kigezo cha dini ni kitendo kinachowapa mashaka.
Kwa upande waratibu wa Mtandao wa Jukwaa la utu wa mtoto,Mkurugenzi wake Konsuma Mtengeti,amesema vita dhidi ya umasikini haiwezi kumalizwa nchini endapo mtoto ataolewa chini ya miaka 18
Mtandao wa TECMN umeliomba Bunge kufanya marekebisho ya sheria ya ndoa ya mwaka 1971 ambayo mahakama ya Rufani mwaka 2019 iliamuru Bunge kufanya hivyo na kusahihisha vifungu vya 13 na 17 na kuweka miaka 18 kama umri unaostahili kwa ndoa kwa wavulana na wasichana,kutoka miaka 14 ya sasa ambapo msichana anaweza kuolewa kwa idhini ya mahaka na miaka 15 kwa idhini ya wazazi.