TANZANIA YAJIPANGA KUWA KINARA WA UCHUMI WA BULUU AFRIKA






Na Lilian Ekonga.....

Dar es Salaam, 10 Septemba 2025 – 


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeonesha dhamira ya dhati ya kuimarisha sekta ya Uchumi wa Buluu, ikilenga kuifanya nchi kuwa kinara wa barani Afrika kupitia kongamano kubwa la kitaifa lililowakutanisha wadau kutoka pande zote za Muungano pamoja na washirika wa kimataifa.


Akifungua rasmi kongamano hilo lililofanyika jijini Dar es salaam , Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Bw. Abdallah H. Mitawi, amesema  kuwa Tanzania imejaaliwa rasilimali za baharini na maji ya ndani ambazo zinaweza kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi iwapo zitatumika kwa tija, kwa kuzingatia usimamizi endelevu wa mazingira.


 “Tuna fursa kubwa kupitia ukanda wa pwani wenye urefu wa kilomita 1,424, Ukanda wa Kiuchumi wa Kipekee (EEZ) wenye ukubwa wa zaidi ya kilomita za mraba 223,000, pamoja na rasilimali kama misitu ya mikoko, miamba ya matumbawe, na bandari zaidi ya 900,” alieleza Bw. Mitawi.




Kongamano hilo limeratibiwa kwa ushirikiano kati ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Wizara ya Uchukuzi kupitia Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI), na Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi ya Zanzibar. Limejumuisha wataalamu wa mazingira, wanataaluma, wawekezaji, na wadau kutoka sekta binafsi.


Katika hotuba yake, Bw. Mitawi alitaja uvuvi haramu, uchafuzi wa mazingira, ukosefu wa teknolojia, na uelewa mdogo wa wananchi kuwa ni changamoto zinazoathiri maendeleo ya sekta hiyo. Hata hivyo, alieleza matumaini kuwa kupitia jukwaa hilo la kitaifa, suluhisho la changamoto hizo litaweza kupatikana kwa ushirikiano wa karibu kati ya sekta ya umma na binafsi.



Aidha, alisisitiza ushiriki wa vijana, wanawake na sekta binafsi katika uendelezaji wa uchumi wa buluu, huku akitoa wito wa ushirikiano mpana wa kitaifa na kimataifa katika kutekeleza ajenda hiyo. 


“Serikali ipo tayari kushirikiana na wadau wote kuhakikisha Tanzania inakuwa kinara wa uchumi wa buluu barani Afrika,” alisisitiza.



Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es salaam  (DMI) Prof. Tumaini Gurumo amesema kongamano hilo lina lengo la kujadili changamoto na kuona namna ya kupata utatuzi  ili zisiwe kikwazo katika ukuwaji wa blue wa nchini.


Ameongeza kuwa Kauli Mbiu ya Kongamano hilo  ni, Bahari yetu, Fursa yetu na Wajibu wetu, na  litakuwa la siku mbili katika kujadili na kuangalia mustakabali wa namna wataweza kukuza  uchumi wa Blue kwa manufaa ya taifa letu.





Previous Post Next Post