Dar es Salaam, Septemba 11, 2025
Na Lilina Ekonga...
Katibu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbas, ametoa wito kwa wadau wa maendeleo, wakiwemo Shirika la Uhifadhi wa Mazingira Duniani (WWF), kuendelea kushirikiana na serikali katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi na kulinda rasilimali za misitu nchini.
Dkt. Abbas alitoa wito huo jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya upokeaji na uzinduzi wa vifaa vya usimamizi wa misitu na huduma za ugani na uenezi, vilivyotolewa kupitia Mradi wa Mbinu za Pamoja za Upatikanaji wa Nishati, unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya kupitia WWF.
"Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kulinda rasilimali misitu, ikiwemo kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa uhifadhi na athari za uharibifu wa misitu. Tunakaribisha WWF na wadau wengine kuendelea kushirikiana nasi katika kukabili changamoto hizi, hasa zile zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi," alisema Dkt. Abbas.
Kwa upande wake, Kamishna wa Uhifadhi, Prof. Dos Santos Silayo, alieleza kuwa serikali imejipanga kuhakikisha usimamizi madhubuti wa maeneo ya hifadhi sambamba na kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala, ili kupunguza utegemezi wa nishati ya mimea ambayo ni chanzo kikuu cha uharibifu wa misitu.
"Takwimu zinaonyesha kuwa takriban asilimia 75 ya kaya nchini bado zinatumia nishati ya mimea. Lengo letu ni kuimarisha matumizi ya nishati safi na salama, sambamba na kuendeleza kampeni ya matumizi ya nishati safi ya kupikia inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan," alieleza Prof. Silayo.
Naye Mkurugenzi wa WWF Tanzania, Dkt. Amani Ngusaru, alisema shirika hilo limekuwa likisaidia shughuli za uhifadhi nchini kwa zaidi ya miaka 30, na kwamba wako tayari kuendelea kushirikiana na serikali katika kujenga uwezo wa wadau wa uhifadhi ili kuhakikisha maeneo ya hifadhi yanalindwa kwa ufanisi.
Akielezea kuhusu mradi huo, Afisa Mradi, Savinus Kessy, alisema mradi unalenga kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya nishati kwa kuimarisha uzalishaji, pamoja na kuboresha miongozo ya uhifadhi wa asili na utendaji wa taasisi zinazohusika na usimamizi wa misitu.
Mradi huo umegharimu zaidi ya shilingi bilioni moja na umewezesha ununuzi wa vifaa mbalimbali vya kusaidia uhifadhi ikiwemo pikipiki, magari, boti ya mwendokasi, vifaa vya TEHAMA, jenereta, pamoja na mifumo ya usimamizi na ufuatiliaji wa misitu.