*WAKATI TRA IKIDAI BILIONI 4.7 ZA KODI, CRC WAKIMBILIA TENA MAHAKAMANI KUZUIA MNADA*







-Wakili Alex Mgongolwa avaa viatu vilivyomshinda Mwalongo vya kutaka kutumia mahakama kama kichaka cha kukwepa kulipa Kodi, Madeni*


Na. Mwandishi wetu,


Wakati Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) ikiendelea kudai Shilingi bilioni 4.7 za malimbikizo ya kodi kutoka kwa kampuni ya Continental Reliable (Tanzania) Limited (CRC), kampuni hiyo imeibukia tena mahakamani katika jaribio jipya la kuzuia mnada wa mali zake uliopangwa kufanyika ili kufidia madeni yake.


Hatua hiyo inakuja siku chache baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania kutupilia mbali maombi ya CRC yaliyokuwa yakipinga hatua za benki za Equity Bank Kenya na Equity Bank Tanzania kudai marejesho ya mkopo unaofikia Shilingi bilioni 26, na kuiagiza kampuni hiyo kulipa madeni hayo.


Kufuatia uamuzi huo, mali za CRC zilipangwa kupigwa mnada wa njia ya zabuni kupitia kampuni ya udalali ya Adili Auction Mart Limited, hatua inayolenga kufidia deni la benki pamoja na kuwezesha serikali kukusanya kodi inayodaiwa.


Katika hatua hiyo, TRA iliielekeza kampuni ya udalali wa mahakama ya Adili kuwa inaidai CRC zaidi ya Shilingi bilioni 4.7 kama malimbikizo ya kodi.


Mamlaka hiyo pia ilielekeza kuwa baada ya kukamilika kwa mnada wa mali za kampuni hiyo, dalali huyo akate kiasi hicho cha fedha kutoka katika mapato yatakayopatikana na kukilipa TRA kama malipo ya kodi zilizochepushwa na kampuni hiyo.  


Hata hivyo, katika hali ya kushangaza, wakati hatua hizo zikiendelea, CRC imeibukia tena mahakamani — safari hii katika Mahakama ya Rufaa ya Tanzania — ikiomba zuio la utekelezaji wa zoezi la mnada wa mali zake.


Kwa mujibu wa taarifa za uhakika kutoka mahakamani, kampuni hiyo imefungua shauri jipya ikiomba kusimamishwa kwa utekelezaji wa mnada huo ambao kukamilika kwake kungewezesha kurejeshwa kwa mabilioni ya fedha zinazodaiwa na benki pamoja na kodi za serikali ambazo ni mapato ya Watanzania.


Taarifa hizo zinaeleza kuwa CRC imeonyesha haraka ya kipekee katika shauri hilo hadi kufikia hatua ya kulazimisha kesi hiyo kuitwa leo, huku wahusika katika shauri hilo wakitajwa kupewa taarifa kwa njia ya simu badala ya utaratibu wa kawaida wa mahakama wa kusambaza taarifa rasmi.


Katika maombi hayo mapya, CRC imeachana na wakili Frank Mwalongo aliyekuwa akiiwakilisha hapo awali na safari hii imemteua wakili Alex Mgongolwa kuendesha maombi hayo katika Mahakama ya Rufaa.


Hatua hiyo imeibua mjadala miongoni mwa wachambuzi wa sheria na uchumi kuhusu matumizi ya mifumo ya mahakama katika migogoro ya kifedha, hasa pale wadaiwa wakubwa wanapotumia hatua za kisheria kuchelewesha ulipaji wa madeni ya benki pamoja na kodi za serikali ambazo ni mapato muhimu kwa maendeleo ya nchi.

Previous Post Next Post