Na Lilian Ekonga, Dar es salaam
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, ametoa wito kwa sekta binafsi nchini kushirikiana na vyuo vya elimu ya juu na ufundi kwa kuwekeza katika tafiti, hususan za sayansi na teknolojia, ili kuinua viwango vya tafiti, kuboresha ubora wa elimu na kuongeza fursa za ajira kwa vijana.
Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati wa uzinduzi wa Mpango wa Ushirikiano kati ya Taasisi za Elimu na Waajiri uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam. Amesema kupitia mpango huo, sekta binafsi itakuwa na nafasi ya kuchangia maendeleo ya elimu kwa kufadhili tafiti pamoja na kutoa ufadhili kwa wanafunzi wa fani mbalimbali kulingana na mahitaji halisi ya soko la ajira.
Aidha, Makamu wa Rais amezitaka taasisi za elimu na sekta binafsi kuzingatia kasi ya maendeleo ya sayansi na teknolojia duniani katika utekelezaji wa mpango huo. Amesisitiza umuhimu wa vyuo na waajiri kushirikiana kubaini ujuzi unaohitajika kwa sasa na siku zijazo, hususan katika fani za sayansi, teknolojia, ubunifu, tiba, uhandisi na hesabu, ili kuwawezesha vijana kushindana katika soko la ajira la ndani na kimataifa.
Ameongeza kuwa ushirikiano kati ya taasisi za elimu na viwanda ni hitaji la lazima katika dunia ya leo, akieleza kuwa vyuo haviwezi kuendelea kuwa vituo vya nadharia pekee, na viwanda haviwezi kukua bila nguvukazi yenye ujuzi unaoendana na teknolojia na ushindani wa soko.
Makamu wa Rais amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeweka kipaumbele cha kimkakati katika kukuza ujuzi, stadi, maarifa na sifa za kuajirika au kujiajiri miongoni mwa vijana na wahitimu wa ngazi zote za elimu, ikitambua kuwa maendeleo endelevu ya Taifa hayawezekani bila kuwa na rasilimaliwatu iliyoelimika na yenye uwezo wa kuchangia kikamilifu katika uchumi wa Taifa.
Uzinduzi wa mpango huo ni utekelezaji wa ahadi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliyoitoa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, ambapo aliahidi kuanzisha mpango wa pamoja kati ya waajiri, vyuo vya ufundi stadi na vyuo vikuu kwa lengo la kulinganisha mafunzo na mahitaji halisi ya sekta za kipaumbele za Taifa ndani ya siku 100 baada ya kuapishwa kwake.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema mpango wa kitaifa wa kukuza ujuzi na ajira umetayarishwa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo Vyuo vya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), waajiri pamoja na wataalamu wa uboreshaji wa mitaala, akisisitiza kuwa ushirikiano huo ni msingi wa kuhakikisha wahitimu wanapata ujuzi unaohitajika katika soko la ajira.
Prof. Mkenda ameongeza kuwa mafanikio ya ushirikiano kati ya taasisi za elimu na viwanda tayari yameanza kuonekana, ambapo wahitimu wa VETA, hususan VETA Moshi, wamekuwa wakipata ajira ndani na nje ya nchi, ikiwemo Namibia, Guinea-Conakry, Mauritania, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Ghana.
Amesema uzinduzi wa mpango huo utaongeza ushirikiano kati ya waajiri na taasisi za elimu, kuwahamasisha wazazi kuwapeleka watoto wao katika vyuo vya ufundi ili kupata ujuzi, na hatimaye kuchangia katika kukuza uchumi wa Tanzania.




