MKUTANO WA NNE WA KITAIFA WA KILIMO IKOLOJIA HAI WAAHIRISHWA, KUFANYIKA MACHI 2026 DODOMA



Na Mwandishi Wetu Dar es salaaam


 Shirika la Kilimo Hai Tanzania (TOAM) kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, limetangaza kuahirishwa kwa Mkutano wa Nne wa Kitaifa wa Kilimo Ikolojia Hai (IV NEOAC), ambao sasa unatarajiwa kufanyika kuanzia Machi 03 hadi 05, 2026 katika Jiji la Dodoma.


Hapo awali, mkutano huo ulipangwa kufanyika Januari 27 hadi 29, 2026, lakini umeahirishwa ili kutoa nafasi ya maandalizi ya kina zaidi na kuwezesha ushiriki mpana wa wadau muhimu kutoka ndani na nje ya nchi.


Akizungumza kuhusu mabadiliko hayo, Mkurugenzi Mkuu wa TOAM, Bw. Bakari Mongo, alisema kuwa uamuzi wa kuahirisha mkutano huo umezingatia umuhimu wa kuhakikisha ubora, ufanisi na matokeo chanya ya tukio hilo.


“Tunawashukuru wadau wetu kwa uvumilivu na uelewa wao. Tarehe hizi mpya zinatupa fursa ya kuandaa mkutano wenye ubora zaidi na programu iliyoimarishwa itakayochangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya Kilimo Ikolojia Hai nchini Tanzania na Afrika kwa ujumla,” alisema Bw. Mongo.



Aliongeza kuwa TOAM inaomba radhi kwa wadau wote kwa usumbufu wowote uliosababishwa na mabadiliko ya tarehe, na imewahakikishia kuwa maandalizi yanaendelea kwa kasi ili kuhakikisha mkutano huo unakuwa na matokeo chanya, endelevu na yenye tija. Alibainisha kuwa taarifa zaidi kuhusu programu iliyoboreshwa, orodha ya wasemaji na taratibu za usajili zitatolewa kupitia tovuti rasmi ya mkutano.


Mkutano wa IV NEOAC unatarajiwa kuwakutanisha wadau takribani 400, wakiwemo wakulima, watunga sera, watafiti, wasomi, wawakilishi wa sekta binafsi, asasi za kiraia, wabia wa maendeleo pamoja na wanahabari. Kupitia mkutano huo, washiriki watapata fursa ya kubadilishana maarifa na uzoefu kwa lengo la kuimarisha mifumo endelevu ya uzalishaji wa chakula, kulinda mazingira na kuongeza kipato cha wakulima wadogo.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi wa Mtandao wa Mwamvuli wa Kilimo Hai Tanzania (TOAM), Bi. Mwatima Juma, alisema mkutano huo ni jukwaa muhimu kwa mustakabali wa kilimo endelevu nchini.



“IV NEOAC ni fursa muhimu ya kitaifa ya kuimarisha mijadala ya sera, teknolojia na mifumo ya uzalishaji wa chakula endelevu, huku tukishirikiana kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha usalama wa chakula,” alisema Bi. Mwatima.


Maudhui makuu ya mkutano huo ni “Kilimo Ikolojia Hai kwa Mifumo Endelevu ya Chakula”, ambapo majadiliano yataangazia masuala ya usalama wa chakula na lishe, mbinu na teknolojia za kilimo ikolojia hai, ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, manufaa ya kiuchumi kwa wakulima pamoja na mazingira ya sera katika kuendeleza sekta ya kilimo.


Naye Mwakilishi wa SWISSAID Tanzania na mdhamini wa mkutano huo, Bi. Gladness Martin, alisema kuwa wadau wamekubaliana kwa pamoja kuwa kuahirishwa kwa mkutano huo ni hatua muhimu ya kuandaa tukio hilo kwa ukubwa na ubora zaidi.



Aliongeza kuwa kutokana na uzito na umuhimu wa mkutano huo, SWISSAID imeamua kushirikiana katika kuutangaza mkutano huo ndani na nje ya nchi, hususan kwa lengo la kuibua mijadala yenye tija kuhusu masuala ya kilimo na maendeleo endelevu. Aidha, alisisitiza kuwa wanatambua na kuthamini juhudi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuendeleza sekta ya kilimo na kuweka mazingira rafiki ya mijadala ya maendeleo.


Kwa upande mwingine, Charles Bupamba, Mwanachama wa Taasisi ya TOAM, aliwahimiza wadau kuongeza juhudi katika kufuatilia na kuelewa kwa kina masuala ya kilimo ikolojia hai, pamoja na kushiriki kikamilifu katika kongamano hilo ili kupata fursa ya kujifunza kwa undani na kusaidia kusambaza maarifa yanayohusiana na sekta ya kilimo kwa jamii pana.


Previous Post Next Post