Wahasibu, Wakaguzi wahimizwa kuwa waadilifu kwa maslai ya Taifa



Na Mwandishi wetu

NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Jenifa Omolo, amewataka wahitimu wa taaluma ya uhasibu na ukaguzi wa hesabu nchini kuzingatia maadili, uadilifu na uaminifu katika utendaji wao wa kazi kwa kufuata miongozo ya kisheria iliyowekwa na mamlaka husika ni msingi muhimu wa kujiepusha na vitendo vya rushwa na ukiukwaji wa maadili ya taaluma.

Akizungumza katika mahafali ya 47 ya Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), Omolo amewahimiza wahitimu hao kutekeleza wajibu wao kwa weledi, uwazi na uaminifu, akisisitiza kuwa taaluma ya uhasibu inahitaji uadilifu wa hali ya juu ili kulinda maslahi ya taifa na wananchi.




Aidha, Omolo amesema endapo taaluma hiyo itatumika ipasavyo kwa kuzingatia misingi ya maadili, uaminifu na uadilifu, itachangia kwa kiwango kikubwa kupunguza vitendo vya ufisadi, ubadhirifu wa fedha na matumizi yasiyo sahihi ya rasilimali za umma na kuchangia kwa kiasi kikubwa kukua kwa uchumi nchini.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya NBAA, Profesa Sylvia Temu, amewakumbusha wahitimu kuzingatia miongozo ya utekelezaji wa taaluma hiyo, amesema bodi haitasita kuwachukulia hatua stahiki watakaokiuka maadili au kufanya kazi kinyume na kanuni na sheria za taaluma hiyo.

Baadhi ya wahitimu wa uhasibu na ukaguzi wa hesabu walieleza dhamira yao ya kutumia taaluma hiyo kwa kusimamia weledi na kutekeleza majukumu yao kwa kufuata mwongozo wa sheria. Akizungumza katika mahafali hayo, CPA Vaileth Victus pamoja na CPA Jafar Ogaga walisema wako tayari kutumia ujuzi wao kulinda rasilimali za umma na kuongeza ufanisi katika maeneo watakayopangiwa.


Tanzania inatajwa kuwa miongoni mwa nchi zenye wahitimu wanaokidhi viwango vya kimataifa katika uhasibu na ukaguzi wa hesabu. Wahitimu kutoka nchini wamekuwa wakitambulika na kufanya kazi katika bara la Asia, Ulaya, Marekani na maeneo mbalimbali ya Afrika, jambo linaloonyesha uwezo na ubora wa mafunzo yanayotolewa chini ya NBAA.
Previous Post Next Post