TBA KUTEKELEZA MRADI MKUBWA WA KIMAENDELEO NCHINI



Na Humphrey Msechu, Geita.

Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) umetangaza mpango wa kutekeleza mradi mkubwa wa ujenzi katika siku za karibuni, huku ukiwashukuru viongozi wa serikali kwa kuwezesha mazingira rafiki ya utekelezaji wa miradi hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Afisa Habari wa TBA, Adam Mwingira, alisema hatua hiyo imechochewa na mabadiliko ya kisheria yaliyofanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Sheria ya Majengo GN Namba 595 ya mwaka 2023. Marekebisho hayo yanaruhusu TBA kushirikiana na sekta binafsi pamoja na taasisi za kifedha ili kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa ubora na kwa wakati.

Mwingira alisema kupitia fursa hiyo, TBA inawakaribisha wawekezaji wenye nia ya kushirikiana kwa njia ya ubia ili kuongeza ufanisi na kasi ya ujenzi wa miradi ya kimkakati nchini. Alisisitiza kuwa ushirikiano wa aina hiyo utasaidia kuongeza thamani ya miradi na kuleta manufaa kwa jamii kwa ujumla.


Aidha, aliainisha baadhi ya miradi mikubwa ambayo tayari TBA imeitekeleza, ikiwemo ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Chato na Hospitali ya Mkoa wa Geita, ambazo zimekuwa kichocheo cha kusogeza huduma za afya karibu zaidi na wananchi.

Aliongeza kuwa miradi hiyo imechangia kupunguza changamoto za upatikanaji wa huduma za matibabu kwa wananchi wa maeneo hayo na kuongeza ustawi wa jamii kwa ujumla.

Mwingira pia alitaja kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, akibainisha kuwa ni moja ya vielelezo vya utekelezaji wenye tija unaofanywa na TBA katika kuboresha miundombinu ya umma.

Vilevile, alisema taasisi hiyo inatekeleza miradi mingine ikiwemo ujenzi wa ofisi za Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Kwa mujibu wa TBA, utekelezaji wa miradi hiyo ni sehemu ya mikakati ya serikali ya kusogeza huduma karibu na wananchi na kuhakikisha taasisi za umma zinakuwa na mazingira bora ya kufanyia kazi.

Previous Post Next Post