Na Mwandishi wetu, Geita
Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania ( TASAC ), limewataka wachimbaji wadogo na wakubwa wa madini pamoja na makampuni ya ugomboaji na uondoshaji wa shehena, kuhakikisha kemikali na vilipuzi vinavyotumika kwenye migodi zinaondolewa na wataalam wa TASAC pekee na si vinginevyo.
Agizo hilo limetolewa na Mkurugenzi wa Huduma za Shirika hilo Hamid Mbegu kwenye Maonesho ya Nane ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini, yanayofanyika Mkoani Geita.
Amesema kwa Mujibu wa Sheria, TASAC ndiyo taasisi pekee ya Serikali imepewa jukumu la kipekee la kusimamia masuala yote yanayohusiana na ugomboaji na uondoshaji wa shehena za vilipuzi kama baruti na kemikali zinazotumika katika shughuli za uchimbaji na usafishaji wa madini nchini kwa mujibu wa Sheria ya Uwakala wa Meli, Kifungu Na.7, Sura 415.
"Baadhi ya shehena hizi ni sumu na zenye madhara makubwa, hivyo Serikali kupitia TASAC,inapaswa kusimamia kikamilifu uondoshaji wake. Rai yetu kwa wachimbaji, makampuni ya uagizaji na ya ugomboaji na uondoshaji ni kutambua kwamba jukumu la kuondoa shehena hizi ni la TASAC pekee, wanaopitisha shehena kupitia kampuni binafsi wanakiuka sheria, " amesisitiza.
Kumekuwepo na baadhi ya kampuni ambazo zimekuwa zikisafirisha kemikali hatarishi kama Sodium Cynite, kupitia makampuni binafsi kwa ajili ya shughuli za ulipuaji migodini, jambo ambalo linaelezwa kuwa ni kinyume cha sheria na taratibu.
