FCC NA ZFCC WATIA SAINI MKATABA WA MAKUBALIANO KULINDA MASOKO NA WALAJI

 





Na Mwandishi wetu...

Tume ya Ushindani (FCC) ya Tanzania Bara na Tume ya Ushindani wa Haki Zanzibar (ZFCC) zimetia saini mkataba wa makubaliano wenye lengo la kuhakikisha kuwepo kwa masoko yenye ushindani wa haki na kulinda maslahi ya walaji katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Akizungumza katika hafla ya utiaji saini huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdalah, alisema makubaliano hayo yanaweka msingi thabiti wa utekelezaji wa shughuli za pamoja kati ya taasisi hizo mbili.


 "FCC na ZFCC zinapaswa kuteua watu au timu maalum kwa ajili ya kusimamia utekelezaji wa makubaliano haya. Ndani ya miezi mitatu, au hata chini ya mwezi mmoja, nyaraka muhimu kama ramani ya utekelezaji (roadmap) au mpango kazi zinapaswa kuwa tayari," alisisitiza Dkt. Hashil.



Aidha, alieleza kuwa kila hatua ya utekelezaji lazima iwe na muda maalum wa utekelezaji ili kuwezesha tathmini ya mafanikio au changamoto zitakazojitokeza. Alisisitiza pia umuhimu wa mafunzo kwa watumishi wa taasisi hizo mbili ili kujenga uelewa wa pamoja kuhusu dhamira ya ushirikiano huo.


“Zamiri yetu ni kusimamia, kuratibu na kuwezesha biashara kwa mujibu wa falsafa ya viongozi wetu wakuu; Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ambao wanasisitiza uboreshaji wa mazingira ya biashara,” alifafanua.


Dkt. Hashil pia alipendekeza kuwepo kwa mpango wa tathmini ya utekelezaji wa makubaliano hayo kila robo mwaka au nusu mwaka, ili kuhakikisha utekelezaji wake unaendelea kwa wakati.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Bi. Khadija Ngasongwa, alisema kuwa mkataba huo ni ishara ya mshikamano wa kitasisi na dhamira ya pamoja ya kulinda masoko na haki za walaji pande zote za Muungano.



"Ushirikiano huu ni hatua ya kimkakati inayolenga kuongeza nguvu ya pamoja katika kukabiliana na changamoto kama ushindani usio wa haki na ukiukwaji wa haki za walaji,” alisema Bi. Ngasongwa.

Alibainisha kuwa ushirikiano huo utahusisha kubadilishana taarifa, mafunzo ya pamoja, utafiti, na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa sheria za ushindani na ulinzi wa walaji.


 “Makubaliano haya yatasaidia kuimarisha mshirikiano kati ya taasisi hizi mbili pamoja na serikali zetu mbili, kwa kuhakikisha kuwa masoko yetu yanabaki kuwa ya haki na yenye ushindani,” aliongeza.

Kwa upande wa Zanzibar, Kaimu Mkurugenzi wa ZFCC, Bi. Aliyah Juma, alisema tume hiyo ipo tayari kushirikiana kwa karibu na FCC kuhakikisha utekelezaji wa makubaliano hayo unafanyika kwa ufanisi.






 “Lengo kuu ni kuhakikisha changamoto zote zilizopo katika masoko zitatuliwe kwa pamoja, na kuhakikisha ushindani wenye tija na haki kwa pande zote za Muungano,” alisema Bi. Aliyah.


Aliahidi kuwa ZFCC itakuwa bega kwa bega na FCC kuhakikisha kila kipengele cha makubaliano hayo kinatekelezwa kwa weledi.



Previous Post Next Post