BoT yahimiza wachimbaji wa dhahabu kujiunga na mfumo rasmi wa kifedha wa kuuza dhahabu zao



Na Humphrey Msechu, Geita

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imewataka wachimbaji wa madini, hususan wa dhahabu, kujiunga na mfumo rasmi wa kifedha kwa kuuza dhahabu zao moja kwa moja kwa Benki Kuu ili kusaidia kukuza akiba ya fedha za kigeni na kuimarisha uchumi wa taifa.

Meneja wa Uhusiano wa Umma na Itifaki wa BoT, Victoria Msina, alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akimpa maelezo Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, alipotembelea banda la BoT katika Maonesho ya Nane ya Madini yanayomalizika leo Septemba 28, 2025 mkoani Geita.

Msina alisema BoT imejikita katika kununua dhahabu kutoka kwa wachimbaji wadogo na wa kati sambamba na kuwaelimisha kuhusu matumizi sahihi ya mifumo ya kifedha, ikiwemo uwekezaji katika dhamana za serikali kwa lengo la kuongeza ushirikiano kati ya sekta hiyo na taasisi za kifedha.

Aidha, alibainisha kuwa elimu hiyo inatolewa katika vituo mbalimbali vya BoT vilivyopo nchini pamoja na kupitia maonyesho na mikutano ya sekta ya madini, hatua inayolenga kuwakwamua wachimbaji kutoka kwenye mifumo isiyo rasmi.

Katika maonesho hayo, wachimbaji kutoka maeneo mbalimbali walijitokeza kutembelea banda la BoT ambapo walipata maelezo na ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya kifedha yanayohusu biashara ya madini.

“Tunawasihi waje tuwafundishe kwa sababu wakielewa mfumo huu, wataweza kujiinua kiuchumi na kuiwezesha serikali kutekeleza miradi ya maendeleo kupitia uwekezaji wao kwenye dhamana,” alisema Msina.

Aliongeza kuwa BoT inatoa pia elimu ya fedha kwa wachimbaji juu ya namna bora ya kukopa kwa malengo, matumizi sahihi ya fedha na matumizi ya mifumo rasmi ya malipo inayosimamiwa na benki hiyo. “Unakopa kwa malengo, si kwa kununua vitu visivyo na maendeleo,” alisisitiza.

Benki Kuu ya Tanzania inatarajia kupitia ushirikiano huo wachimbaji wa madini watachangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha uchumi wa taifa pamoja na kujikwamua kiuchumi binafsi kupitia maarifa ya kifedha na uwekezaji rasmi.

Previous Post Next Post