Katibu Mkuu Kiongozi Zanzibar Mhe. Zena aipongeza BOT Kwa kuzidi kutoa elimu ya FEDHA Kwa Wananchi



Na Humphrey Msechu, Geita

Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Zena Ahmed Said, amepongeza jitihada za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kutoa elimu ya fedha kwa wananchi kupitia banda lake katika Maonyesho ya Nane ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini Mkoani Geita. Akizungumza baada ya kutembelea banda hilo, Zena alisema elimu hiyo ni muhimu kwa ustawi wa kiuchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla.

Katika banda hilo la BoT, wananchi walipata mafunzo ya namna bora ya kuwekeza fedha zao, hasa kwenye dhamana za Serikali, ambazo zimeelezwa kutoa faida kubwa na salama kwa wawekezaji. Katibu Mkuu Kiongozi alisema kuwa elimu hii itasaidia wananchi wenye fedha kutambua njia sahihi za kuzitumia kwa maendeleo yao na ya taifa.

“Kuna watu wana fedha zao nyingi lakini hawajui jinsi ya kuziwekeza. Kupitia elimu hii, sasa wanaweza kuelekezwa kuwekeza kwenye dhamana za Serikali ambazo ni salama na zenye tija,” alisema Zena.


Mbali na elimu ya uwekezaji, BoT pia inatoa mafunzo kuhusu namna ya kujiepusha na vitendo vya utakatishaji wa fedha, ambacho ni tatizo la kimataifa linaloweza kuiingiza nchi kwenye matatizo ya kifedha na kisheria. Zena alisema elimu hii itawasaidia wananchi kuelewa madhara ya kushiriki au kuhusishwa na vitendo hivyo haramu.

Aidha, alieleza kuwa masuala mengine ya kifedha yanayotolewa katika banda la BoT ni pamoja na mbinu za kusimamia fedha za kaya, kuweka akiba, na kuongeza maarifa ya kifedha kwa wajasiriamali wadogo na wa kati. Alisisitiza kuwa elimu hiyo inawawezesha wananchi kufanya maamuzi ya kifedha kwa ujasiri na ufanisi.

Zena aliongeza kuwa maonyesho hayo hayakubaki tu kwa wachimbaji na wadau wa sekta ya madini, bali pia yamewaunganisha wajasiriamali kutoka Tanzania Bara, Visiwani na hata nje ya mipaka ya nchi. Kwa mujibu wake, ushirikishwaji huo ni fursa ya kipekee ya kujenga mtandao mpana wa kibiashara na ushirikiano wa maendeleo.


Kwa upande wake, BoT imeendelea kusisitiza dhamira yake ya kuhakikisha wananchi wanapata uelewa mpana kuhusu huduma zake na nafasi yake katika kukuza uchumi wa taifa. Wawakilishi wa benki hiyo walisema elimu ya fedha kwa wananchi ni nyenzo muhimu ya kupunguza umasikini na kuongeza usawa katika fursa za kiuchumi.

Kwa ujumla, Katibu Mkuu Kiongozi alifurahishwa na maonyesho hayo na kupongeza ubunifu wa wadau wote waliotoa nafasi ya kuelimisha na kuhamasisha wananchi. Alisema hatua hiyo inasaidia si tu sekta ya madini bali pia kukuza uchumi jumuishi unaogusa kila mtanzania.
Previous Post Next Post