Na Humphrey Msechu,Geita
Mkuu wa Wilaya ya Geita, Hashim Komba, ametoa rai kwa Bodi ya Bima ya Amana kuendelea kupanua wigo wa huduma zake ili kuhakikisha mitaji ya Watanzania, hususan katika vikundi vidogo vya kifedha kama SACCOS na VICOBA, inabaki salama. Akizungumza mjini Geita, Komba alisema Watanzania wengi bado wanawekeza fedha katika maeneo ambayo hayajasajiliwa rasmi, hali inayowaletea hasara kubwa pale vikundi hivyo vinapovunjika.
Komba alieleza kuwa katika ofisi za wakuu wa wilaya, mara kwa mara wananchi wamekuwa wakifika kulalamikia kupoteza akiba kubwa walizowekeza. “Unampokea mwananchi anakwambia amewekeza milioni 30 kwenye kikundi cha kifedha lakini zote zimepotea. Tunaanza kuhangaika kumtafuta kiongozi wa kikundi bila mafanikio. Ni wakati sasa wa kuongeza kasi ya kuhakikisha mitaji ya Watanzania inalindwa,” alisema.
Ameongeza kuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inapaswa kushirikiana kwa karibu na Bodi ya Bima ya Amana kushuka chini kwa kasi kubwa ili kufikia taasisi ndogo ndogo.
Kwa upande wake, Mkuu wa kitengo cha Uhusiano wa Umma na Mawasiliano wa Bodi ya Bima ya Amana, Lwaga Mwambande, amesema Kwa niaba ya DIB amepokea ushauri wa Mkuu wa Wilaya ya Geita na kusisitiza kuwa ushirikiano na wadau wengine wa sekta ya fedha utaendelea kuimarishwa kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanakuwa na imani katika mfumo rasmi wa kifedha nchini.
Mwambande alifafanua kuwa kwa sasa kinga inayotolewa na bodi hiyo ni Shilingi milioni 7.5 kwa kila mteja endapo benki itafungwa. “Kinga hii inawafikia wananchi wengi kwani asilimia 99 ya wenye amana wanalindwa. Hii inatupa nafasi ya kuendelea kuwahakikishia Watanzania usalama wa fedha zao katika taasisi za kifedha zilizosajiliwa,” alieleza.