NEC YASISITIZA UMUHIMU WA KUFUATA SHERIA NA KATIBA KATIKA UCHAGUZI




Na mwandishi wetu......

Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Mheshimiwa Balozi Omar Ramadhan Mapuri, amesisitiza umuhimu wa kufuatwa kwa taratibu na hatua mbalimbali za kikatiba na kisheria ili kuhakikisha mchakato wa uchaguzi unakuwa wa haki, amani na usalama.

Leo Julai 21, 2025, mkoani Dar es Salaam, Balozi Mapuri alizindua mafunzo kwa watendaji wa uchaguzi kutoka mikoa ya Dar es Salaam na Pwani. Mafunzo hayo yanahusisha waratibu wa uchaguzi, wasimamizi wa uchaguzi, wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya jimbo, maafisa wa uchaguzi pamoja na maafisa wa ununuzi, na yanatarajiwa kuendelea hadi Julai 23, 2025.

Akifungua mafunzo hayo, Balozi Mapuri alisisitiza kuwa, ili kuepuka malalamiko au vurugu zinazoweza kutokea wakati wa mchakato wa uchaguzi, ni muhimu kwa watendaji wote kufuata hatua za kikatiba na kisheria zilizowekwa. Aliongeza kuwa, mafunzo haya ni muhimu kwa kuhakikisha kuwa watendaji wa uchaguzi wanakuwa na uelewa mzuri wa majukumu yao na kwamba watashirikiana ipasavyo katika kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa usawa na haki.

“Mchakato wa uchaguzi ni jumuia ya jamii nzima na hivyo ni muhimu kwa kila mmoja wetu kuzingatia sheria na taratibu ili kuepuka migogoro yoyote inayoweza kujitokeza. Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ina jukumu la kuhakikisha kuwa kila uchaguzi unafanyika kwa ufanisi na kwa kuzingatia haki za kila mpiga kura,” alisema Balozi Mapuri.

Mafunzo kama hayo yanafanyika kwa wakati mmoja katika mikoa mingine ya Shinyanga, Mwanza, Rukwa, Mbeya, Kaskazini Pemba na Kusini Pemba, ambapo watendaji wa uchaguzi wa mikoa hiyo pia wanapata mafunzo ya namna bora ya kusimamia uchaguzi na kuzingatia taratibu za kisheria.

Katika hatua nyingine, Balozi Mapuri aliwakumbusha watendaji wa uchaguzi kuwa, ni muhimu kuhakikisha kuwa wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu mchakato wa uchaguzi na kwamba watendaji hao watachukua hatua za haraka endapo kutatokea changamoto yoyote ili kuepusha madhara zaidi.

Pia, alifafanua kuwa ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha uchaguzi wa haki unafanyika bila kuvuruga utulivu wa taifa, kwani mchakato mzuri wa uchaguzi unahakikisha kwamba sauti ya kila raia inasikika na inaheshimiwa.

Mafunzo haya yana lengo la kuboresha ufanisi wa uchaguzi katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani, huku wakitarajia kupata wataalamu watakaowezesha mchakato wa uchaguzi kuwa na ufanisi na usalama wa hali ya juu.
Previous Post Next Post