Katika juhudi za kuharakisha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia nchini, Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kushirikiana na Shirika la Taifa la Madini (STAMICO), wameingia katika makubaliano ya kujenga kiwanda kipya cha kuzalisha mkaa mbadala (Rafiki Briquettes) mkoani Geita.
Mradi huo mkubwa utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 4.5 na unalenga kuleta suluhisho endelevu kwa changamoto ya utegemezi wa mkaa wa miti na kuni majumbani.
Katika hafla ya utiaji saini iliyofanyika leo julai 2w kwenye Ofisi Ndogo ya REA jijini Dar es Salaam, pande zote mbili zilieleza kuwa fedha hizo zitatolewa kwa mgawanyo wa shilingi bilioni 3 kutoka REA, na shilingi bilioni 1.5 kutoka STAMICO. REA itahusika na ununuzi wa mashine za uzalishaji, huku STAMICO ikigharamia upatikanaji wa eneo la ujenzi, ujenzi wa miundombinu ya kiwanda pamoja na kazi ya ufungaji wa mitambo.
Mkataba huo ulisainiwa rasmi na Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt. Venance Mwasse.
Kiwanda hiki kitakuwa ni cha tano kwa STAMICO katika juhudi zake za kuongeza uzalishaji wa nishati mbadala nchini. Kwa sasa, viwanda vingine vinavyofanya kazi ya kuzalisha mkaa mbadala vipo katika maeneo ya Kisarawe (Pwani), Kiwira (Songwe), na viwanda viwili vilivyopo mkoani Dodoma na Tabora ambavyo vinakaribia kuanza uzalishaji rasmi.
Akizungumza katika tukio hilo, Mhandisi Saidy amesema kuwa REA imepewa jukumu la kuhakikisha Watanzania wanapata nishati safi ya kupikia kwa asilimia 80 ifikapo mwaka 2034. Aliongeza kuwa Wakala unatekeleza miradi kadhaa kwa lengo la kuongeza uzalishaji na usambazaji wa nishati safi, hususan vijijini.
“Mkataba huu ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye amesisitiza mashirika ya serikali kushirikiana ili kuongeza upatikanaji wa nishati safi kwa wananchi na kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa wa miti,” alisema Mhandisi Saidy.
Kwa upande wake, Dkt Venance Mwasse, Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO ameishukuru Serikali kupitia REA kwa mchango huu ambao utasaidia Shirika hilo kutimiza ndoto yake ya kuhakikisha wananchi wote wanaachana na nishati isiyo safi na salama ya kupikia ifikapo mwaka 2034 na hivyo kuunga mkono juhudi za Serikali za kutunza mazingira.
“Hii ajenda ya matumizi ya nishati safi ambayo kinara wake ni Rais wa Awamu ya Sita, Dkt. Samia Suluhu Hassan inalenga kumkomboa Mwanamke ili aachane na nishati isiyo safi na salama. STAMICO tumejipanga kutekeleza maono haya ya Kiongozi wetu”, amesema Dkt. Mwasse.
Ameongeza kuwa nishati ya Rafiki Briquettes kwa sasa inatumiwa na Jeshi la Magereza ambapo Magereza yote 129 nchini kote yanatumia nishati hii kama aina mojawapo ya nishati ya kupikia, vikosi vya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) pamoja na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Taasisi nyingine ni pamoja na vyuo mbalimbali vya mafunzo, shule za msingi na sekondari, hoteli, migahawa, na sehemu wanazochoma nyama na chipsi.
Dkt. Mwasse amesisitiza kuwa STAMICO itaendelea kutunza mitambo hiyo ili iendelee kutoa huduma kwa Wananchi.