Na Mwandishi Wetu Morogoro
BAADHI ya Wananchi wa Jimbo la Uchaguzi la Morogoro Mjini, wamehoji kitendo kinachofanywa na Mbunge wa Jimbo hilo cha kuanza kutoa misaada mbalimbali Jimboni humo zikiwa zimesalia siku chache kabla ya Bunge kuvunjwa rasmi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwa sharti la kutotajwa majina yao kwa hofu ya kujulikana, wananchi hao wamedai kushangazwa na hatua hiyo ya kiongozi huyo wakati huu ambao wabunge wote wamebakiwa na takribani wiki moja ili kumaliza ubunge wao.
"Ukweli hata kama ndiyo utekelezaji wa ahadi alizowahi kuzitoa, hii kwetu ni kama 'janja janja' ya kutusahaulisha maumivu, kwani zipo ahadi ambazo aliwahi kuzitoa miaka saba iliyopita lakini leo ndiyo amekuja kuitekeleza, huu ni sawa mtego wa kutaka tumkumbuke tena" amesema mmoja wa wakazi wa eneo la Msamvu.
Hii inakuja ikiwa ni dakika za 'lala salama kabla ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuanza mchakato wake wa utoaji fomu kwa ajili ya watu wenye nia ya kuwania nafasi za Ubunge na Udiwani kwa ajili ya kupeperusha bendera ya Chama hicho katika uchaguzi Mkuu wa Oktoba Mwaka huu.
Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mbunge huyo na kusambazwa sehemu mbalimbali yakiwemo 'magrupu ya Whatsup', imeonesha kuwa ataanza ziara ya kuzitembelea Kata 10 za jimbo zikiwemo Kata za Bingwa, Tungi, Kingolwia, Mindu, Mkundi, Boma, Kilakala, Mlimani, Uwanja wa Taifa na Mafiga kuanzia leo na kugawa vifaa mbalimbali likiwemo gari la wagonjwa alilolitoa leo katika Kata ya Kingolwira.
"Sisi tunaona kuwa hii ni kama mbinu mpya ya Mbunge huyu kuwafikia wapiga kura kwa kisingizo cha kutekeleza ilani ya Chama, kwani tangu awe Mbunge kwa awamu hii inayoishia ukingoni yapo maeneo hakuwahi kufika kabisa" alisema mtoa taarifa huyo ambaye ni Diwani aliyemaliza muda wake.
Kwa mujibu wa mjumbe huyo katika ziara hiyo Mbunge huyo amekabidhi gari la wagonjwa kwa kituo cha afya cha Kingolwira lenye usajili Na T802, DSU ambalo hata hivyo linadaiwa kuwa lilikuwa likitumika kwa matumizi yake mengine na kwamba amelikabidhi baada ya gari hilo kufanyiwa marekebisho hivi karibuni ikiwemo kulipaka rangi.
Kabla ya kukabidhi gari hilo , inatajwa pia Mbunge huyo ameshawahi kukabidhi ya wagonjwa magari katika vituo vya afya vilivyopo Kata ya Mafiga, Sabasaba, Lukobe na Tungi huku baadhi ya wadau wakiibua hofu zao kuhusu magari hayo kama kweli mhusika alikabidhi na kadi kwa vituo lengwa.
Amesema hatua inatia mashaka kwa kuwa kumekuwa na sintofahamu nyingi ya kupotea kwa magari yanayokabidhiwa na Mbunge huyo gari lililokabidhiwa na Mbunge huyo wakati wa Corona katika kituo cha Kingolwira ambalo baadae lilipotea na halijapatikana hadi leo hadi Sasa ambapo amekabidhi gari jingine kwa kituo hicho Cha Kingolwira.
Amesema siyo Kingolwira tu bali hata magari yaliyokabidhiwa na Mbunge huyo katika Kata za Lukobe na Tungi lilitolewa Mwaka jana, yamepotea na hayajawahi kupatikana hadi leo jambo linaloonesha kuwa Kuna kitu halipo sawa kuhusiana na utaratibu huo wa kukabidhiwa kwa magari hayo.
“Jambo jingine ukiisoma taarifa ya Mbunge, haisemi ni wapi fedha za kutoa misaada hiyo zinatoka kama ni fedha zake za mfukoni au ni za mfuko wa jimbo, maana kwa kipindi sisi kama wadau tumekuwa hatupewi taarifa za fedha za mfuko wa jimbo zinatumikaje, huenda ndizo hizi zinafanya maendeleo ila mtu anasema zinatoka katika mfuko wake" ameongeza
Aidha wamesema kuna umuhimu mkubwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuangalia masula hayo kwa umakini ikizingatiwa kuwa tayari jimbo hilo ambalo Katibu wa wilaya ambaye ndiye msimamizi wa uchaguzi tayari ameonesha upendeleo wa wazi kwa mmoja wa watia nia ambaye kimsingi anaonekana kuvunja kanuni za uchaguzi.