NAIBU WAZIRI NYONGO ASISITIZA USHIRIKANA KATI YA SERIKALI NA WADAU WA MAENDELEO KUFANIKISHA DIRA YA TAIFA 2050



Na Mwandiahi wetu.....

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Stanslaus Haroon Nyongo, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa maendeleo, akihimiza majadiliano badala ya ukosoaji ili kufanikisha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.

Akizungumza katika mkutano wa Asasi za Kiraia (AZAKI) uliofanyika jijini Dar es Salaam, Mhe. Nyongo amesema maoni ya wananchi na wadau mbalimbali yatakuwa msingi wa kuandaa dira hiyo.

Mhe. Nyongo alibainisha kuwa serikali ipo tayari kusikiliza maoni ya kila mmoja ili kuhakikisha Dira 2050 inakuwa halisi na shirikishi. Amesema uzoefu wake kama Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Maendeleo ya Jamii ulimsaidia kuelewa dhamira ya AZAKI katika kutoa maoni yanayolenga kuimarisha maendeleo ya taifa.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Foundation for Civil Society (FCS), Justice Rutenge amepongeza serikali kwa kuwajumuisha wadau wa kiraia katika uandishi wa Dira 2050.



Rutenge ameainisha kuwa kukuza uchumi shindani ndani ya mikoa ni njia muhimu ya kufanikisha maendeleo endelevu, akitolea mfano wa Kenya ambako kaunti zinashindana kwa vigezo vya kuzalisha ajira na kujumuisha makundi ya pembezoni.

Nae Lucas Kifyasi, Mkuu wa Programu za Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, amesema kuwa utekelezaji wa dira hiyo utahitaji kipaumbele katika elimu, hasa kwa kuzingatia mapinduzi ya viwanda yanayotarajiwa kuimarika miaka 25 ijayo. Alisisitiza kuwa elimu na teknolojia ni nguzo muhimu za maendeleo endelevu.

Mkutano huo umeonyesha dhamira ya pamoja kati ya serikali, AZAKI, na wadau wa kimataifa katika kuhakikisha Tanzania inafanikisha malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.





Previous Post Next Post