TUME ya Kurekebisha Sheria Tanzania yaendelea kupokea maoni kwa wananchi kuhusu maboresho ya Sheria nchini


Na Mwandishi Wetu

TUME ya Kurekebisha Sheria Tanzania imekuwa ikipokea maoni kutoka kwa wananchi kwa ajili ya kuboresha utendaji kazi wake ama uboreshaji wa sheria.

Katibu Mtendaji wa Tume hiyo George Mandepo amesema hayo kwenye Maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi yanayoendelea jijini Dodoma.

Amesema, " Kazi ya Tume ni kufanya mapitio ya sheria zote zilizopo Tanzania na kupendekeza marekebisho serikalini katika maeneo ambayo tunabaini kuna upungufu au kuna mgongano au ukizani wa sheria,".

Amesema katika kufanya hivyo huhusisha wadau wa sekta husika na wengine wanaoathirika  na ile sheria ambayo inatungwq au kufanyiwa marekebisho.

" Katika kufanya kazi tume inaweza ikapendekeza marekebisho, ikapendekeza kufutwa kwa sheria lakini ikapendekeza labda kuboreshwa mifumo yetu  ya usimamizi wa sheria ambazo zipo ndani ya serikali yetu," amesema.

Amesisitiza kuwa tume inapofanya mapitio au marekebisho ya sheria inafanya utafiti wa kupitia sheria zilizopo kwa kuangalia mazingira ya sasa, mazingira yaliyosababisha kutungwa kwa sheria  husika na mazingira yajayo.

"Kwa sababu sheria lazima iishi kama mwanadam inaongea, sheria ina matendo yote ambayo yanapeleka kuonekana  sheria inatumika.

"Kwa hiyo tunaangalia pia uzoefu wa ndani ya nchi na wa nchi nyingine , lakini pia tunaangalia athari ambayo sheria husika inaweza ikaleta kiuchumi, kijamii na pia kisiasa," amesema.

Amesema kama tume wanayaangalia hayo  pamoja na kuwahususha wadau.
Previous Post Next Post