TARURA Yaunganisha Kata Mbili Manispaa ya Shinyanga



Na Mwandishi Wetu

Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini Tanzania (TARURA) imejenga daraja ambalo limeziunganisha Kata mbili za Ndala na Kambarage zilizopo Manispaa ya Shinyanga, mkoani Shinyanga.

Kwa muda mrefu kata hizo zilitenganishwa na mto, hivyo kusababisha wakazi wa maeneo hayo kushindwa kufanya shughuli zao za kila siku.

“Siku za nyuma wakati hatujapata kivuko hiki, tulikuwa na changamoto sana, kwa sababu kulikuwa na wakazi wanaotoka Ndala wanakuja Kambarage, lakini pia kuna wakazi wa Kambarage wanakwenda Ndala. Tulikuwa hatuna kivuko na tuna mto mkubwa sana,” amesema Diwani wa Kata ya Ndala, Mhe. Zamda Shaban.
Ameendelea kusema kuwa, kuna watoto ambao wanasomea Ndala na wanaishi Kambarage, pia wanaosomea Kambarage na wanaishi Ndala. Hivyo watoto hao walilazimika kupita mtoni kwa ajili ya kwenda shule.

“Kipindi cha kiangazi kidogo kulikuwa na unafuu, watu wanapita mtoni pamoja na kuwa kuna maji, lakini ikifika masika eneo hilo lilikuwa halipitiki kabisa, ni mpaka wazunguke, njia ambayo walikuwa wakitumia muda mrefu tofauti na kupita katikati ya mto huo,” amefafanua Mhe. Zamda.

Amesema kupatikana kwa kivuko hicho kimewarahisishia wakazi wa Ndala kupata huduma za kijamii kirahisi, kwani huduma nyingi za kijamii kama zahanati na  masoko vipo katika Kata ya Kambarage.
 

Naye, Ustadhi Rashidi Muhimbe ameishukuru serikali kwa kujali hali ya wananchi wake, na hali ya waumini wa Tanzania.

“Kabla ya ujenzi wa daraja hili, tulikuwa na usumbufu mkubwa sana, ikiwemo changamoto ya upatikanaji wa waumini ndani ya misikiti yetu. Ili misikiti au makanisa yapate uhai lazima wapatikane waumini,” amesema Ustadhi Muhimbe.

Amesema kuwa, kutokana na ujenzi wa daraja hilo kwa sasa mahudhurio ya waumini ni mazuri ukilinganisha na ilivyokuwa mwanzoni.
Previous Post Next Post