Balozi Mbundi Makoba watembelea banda la NHC maonesho ya Nanenane


Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki-anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Balozi Stephen Mbundi ni miongoni mwa viongozi waandamizi serikalini ambao wametembelea banda la Shirika la Taifa la Nyumba (NHC).

Mbali na Balozi Mbundi,pia Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Thobias Makoba naye ametembelea banda hilo leo.

Katika maonesho hayo ya Nanenane ambayo Kitaifa yamefanyika katika viwanja vya Nzunguni jijini Dodoma,wataalamu wa NHC wamekuwa wakitoa huduma na elimu kwa umma kuhusu miradi mbalimbali wanayotekeleza nchini.

Miongoni mwa miradi ambayo imekuwa kivutio zaidi kwa wananchi na wadau mbalimbali waliotembelea banda la NHC ni pamoja na Samia Housing Scheme na Seven Eleven (7/11) ambayo utekelezaji wake unakwenda kwa kasi zaidi jijini Dar es Salaam.

NHC ni miongoni mwa mashirika na taasisi za umma ambazo zimeshiriki Maonesho ya Kilimo ya Kimataifa Nanenane 2024 yakiongozwa na kauli mbiu ya "Chagua Viongozi Bora wa Serikali za Mitaa kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi".

Aidha, licha ya kufanyika Kitaifa jijini Dodoma, maonesho hayo yamefanyika katika Kanda ya Nyanda za Juu Kusini jijini Mbeya kwenye Uwanja wa John Mwakangale; Kanda ya Mashariki mjini Morogoro kwenye Viwanja vya Mwl. Julius Kambarage Nyerere;

Kanda ya Kusini mjini Lindi kwenye Viwanja vya Ngongo; Kanda ya Ziwa Magharibi jijini Mwanza katika Viwanja vya Nyamhongolo; Kanda ya Ziwa Mashariki mkoani Simiyu katika Viwanja vya Nyakabindi;

Kanda ya Kaskazini jijini Arusha kwenye Viwanja vya Themi; na Kanda ya Magharibi mjini Tabora kwenye Viwanja vya Fatma Mwasa.

Maonesho hayo yalifunguliwa Agosti 1,2024 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa (Mb).

Aidha,leo Agosti 8, 2024 Maonesho ya Kilimo ya Kimataifa ya Nanenane 2024 yanafungwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan jijini Dodoma, kwenye viwanja vya Nzuguni.
Previous Post Next Post