Na Humphrey Msechu
Kutokana na ufinyu wa muda katika Mkutano wa 10 wa Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali imeshindwa kuwasilisha Bungeni miswada mbalimbali ya marekebisho ya Sheria ukiwemo mswada wa Sheria ya Huduma za Habari namba 12 ya mwaka 2016.
Hayo yamesemwa leo February 7,2023 na Gerson Msigwa, Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali wakati akizungumza na vyombo mbalimbali vya habari nchini.
"Serikali ilikuwa imeshapanga kwenye mkutano huu tuwasilishe muswada wa mabadiliko ya Sheria mbalimbali kwa wabunge ili wakishafanya marekebisho tuendele kuitumia kwa mujibu wa taratibu na sheria"- Gerson Msigwa
"Tulishaweka malengo ya kuwasilisha muswada wa mabadiliko ya Sheria mbalimbali hususani sheria yetu ya huduma za habari endapo kungetokea nafasi lakini tumeshindwa kwa sababu ya ufinyu wa nafasi" amesema Gerson Msigwa
Pia Msigwa amewaondoa hofu wadao wote wa habari nchini na kuwahakikishia kuwa Serikali itawasilisha mswada huu pamoja na mingine katika Mkutano ujao (Mkutano wa 11) wa Bunge.
"Tunatarajia kikao kijacho amacho kitakuwa mwezi April na tutaunganisha kwenye Bunge la bajeti ambapo kwa wakati huo tutawasilisha sasa muswada wetu wa mabadiliko ya Sheria ya huduma za habari"- Msigwa