Na Humphrey Msechu
Waziri wa Habari , Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape, Nnauye ameongoza kikao cha pili na wadau wa Kupata Habri(CoRI) Katika kupitia mapendekezo ya mabadiliko ya sheria.
Kikao hiko kimefanyika leo Novemba 2022 jijini Dar es salaam ambapo waziri amewahakikishia wadau wa habari kukamilisha mchakato wa mabadiliko ya sheria ya habari.
Waziri amesema serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inayo nia ya dhati katika hili na imepokea maoni yao kuhusu marekebisho ya sheria ya Huduma za Habari Na 12 ya 2016.
"Nimekuja mwenyewe kuwasikiliza na imani yangu ni kuona sekta inaendelea kukua,... na tupo kwa ajili ya kufanya mapitio ya mwisho ua mapendekezo ya marekebisho ya sheria ya Huduma za Habari 2016,"amesema Nape.
Nje ya kikao hicho, Deodatus Balile ambaye ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), alisema una muelekeo mzuri kuelekea mabadiliko ya sheria ya habari.
‘‘Kikao kilikuwa kizuri, serikali imeendelea kuonesha dhamira yake ambayo ilikuwa nayo tangu mwanzo. Tumemaliza na serikali inaendelea na hatua zake kabla ya kupelekwa bungeni.
‘‘Suala la mabadiliko ya vipengele vya sheria lina mchakato wake, cha msingi serikali imetoa fursa, na si kutoa peke yake, inaendelea kuchukua hatua,’’ alisema Balile.
Miongoni mwa mapendekezo ya CoRI kwa serikali ni pamoja na mamlaka haya ya Mkurugenzi wa Habari (MAELEZO) yafutwe na kiundwe chombo ambacho pamoja na mambo mengine, kitashughulikia masuala ya usuluhishi yanapotolewa malalamiko dhidi ya chombo cha habari, badala ya kazi hiyo kufanywa na mtu mmoja.
Wadau wanataka marekebisho dhidi ya kifungu cha 6 (e) kinachoelekeza magazeti kupatiwa leseni badala ya usajili wa moja kwa moja.
Pia wadau hao wanapendekeza magazeti yasiendeshwe kwa kupewa leseni, badala yake yapewe usajili wa kudumu au wa muda mrefu, ili kudhibiti changamoto ya ufutwaji holela wa leseni na kuvutia wawekezaji.
Mapendekezo mengine kuhusu sheria hiyo, ni marekebisho dhidi ya kifungu chake cha 7 (2)(b)(lV), kinachoelekeza vyombo vya habari kutangaza au kuchapisha habari na masuala yenye umuhimu kwa taifa, kadiri itakavyelekezwa na serikali, wadai wakieleza kipengele hiki kinaingilia uhuru wa uhariri.
Sheria nyingine zinazolalamikiwa ni Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Huduma za Posta (EPOCA, 2010), Sheria ya Makosa Mtandaoni (2015), Sheria ya Haki ya Kupata Habari (2016) na Kanuni za Maudhui Mtandao (2018) kama zilivyorekebishwa mara kadhaa.
Sheria hizi zina vifungu vinavyofifisha uhuru wa habari nchini hivyo zinahitaji kubadilishwa.
Wadau walioshiriki kikao nicho ni pamoja na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Umoja wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari (MOAT), Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Chama wa Waandishi wa Habari Tanzania (JOWUTA) na MISA- Tanzania.