NAPE: SERIKALI IPO KWENYE MCHAKATO WA KUFANIKISHA MABADILIKO YA SHERIA YA HABARI


Na Humphrey Msechu

Serikali ipo tayari  kupeleka mapendekezo ya sheria ya habari kwa watunga  sheria, baada ya kikao cha wadau  wa habari na serikali kitakachofanyika tarehe 22 Novemba 2022, jijini Dar es salaam. 

Hayo yamesemwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye, wakati akizungumza na uongozi wa Jukwaa la Wahiriri Tanzania (TEF) na Wadau wa Haki ya kupata Habari(CoRI), jijijni Dodoma tarehe 9 Novemba 2022.

Ambapo amesema Serikali ipo  tayari kupeleka mabadiliko ya sheria ya habari bungeni baada ya kikao cha mwisho. 


Hata hivyo amesema serikali ilishindwa kupeleka mapendekezo ya mabadiliko ya sheria ya habari bungeni katika Bunge la Novemba mwaka huu, kwa sababu baadhi ya taratibu hazikukamilika na kuepuka mivutano kutoka kwa wadau wa habari. 

"Haikuwa vyema kupeleka mapendekezo ya sheria ya habari bungeni wakati kuna maeneo wadau wa habari na serikali walikuwa hawajakubaliana na sisi kama serikali hatujakaa kimya, bado tupo vizuri kwenye mchakato huu. Nia ya serikali mpaka sasa bado ni njema" amesema Nape. 


Amesema kuwa Isingefaa kwenda na mabishano bungeni mpaka sasa kuna maeneo ambayo bado hawaja kubaliana na kikao hicho cha mwisho ndio kitatoa mwelekeo wa mapendekezo yote. 

‘‘Sisi kama tupo happy (tunafuraha) na mchakato wa mabadiliko ya sheria ya habari unavyokwenda, lakini pamoja na yote haya, ni vizuri uhuru uliopo tukautumia vizuri,’’ amesema


Na kwamba, pamoja na mchakato wa mabadiliko ya sheria kuwa njiani kukamilika, serikali inaangalia pia uhalisia wa mabadiliko hayo ya sheria na mazingira ya sasa.

Akizungumzia takwa la Rais Samia Suluhu Hassan la kukutana na wanahabari alilolitoa wakati wa Maadhimisho ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani (WPFD), jijini Arusha Nape ameseman wizara ipo mbioni kuandaa mazingira ya Rais Samia kukutana na wanahabari hao.


‘‘Katika Maadhimisho ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani Rais aliagiza wizara kutaka kukutana na wanahabari. Tunafanyia kazi hilo,’’ amesema Nape. 

Kwa upande wake Gerson Msigwa, Msemaji wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), alishauri wanahabari kubaki Pamoja kwenye mchakato wa mabadiliko ya sheria ya habari.

‘‘Tutumie vizuri kipindi hiki ambacho serikali imekuwa tayari kusikiliza. Tubaki Pamoja mpaka mwisho,’’amesema  Msigwa.


Nae Deodatus Balile, Mwenyekiti wa TEF aliomba wadau wa habari kushiriki vema katika kikao cha mwisho cha serikali na wadau wa habari kwa kuwa ni muhimu.

‘‘Kama kuna mtu anawazo, alilete kupitia umoja wa haki ya kupata habari ili kwenye kikao hicho tuwe na lugha moja,’’ amesema

Nae Dk. Rose Reuben, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) amesema, wadau wa habari wanapaswa kutoa mawazo yao ili ifike mahali wakubaliane katika utungaji wa sheria.


‘‘Tunapaswa kutoa mawazo yetu lakini ili tufike mahali ambapo tunaweza kukubaliani ili kuufanya huu mchakato wa mabadiliko ya sheria uende haraka. Sheria itakapoanza kufanya kazi, tutaanza kuona mabadiliko katika uandishi wa habari ambao ni wakitaaluma,’’ amesema

James Marenga, Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA-TAN), alisema katika kikao cha pili, hakuna jambo litalobaki bila kushughulikiwa.

‘‘Baada ya kikao cha pili kama ambavyo imeelezwa na serikali, tunaamini mabadiliko yatakayopelekwa bungeni yatakidhi matakwa ya wanahabari kwa ajili ya kunufaishi wananchi, serikali na tasnia kwa ujumla,’’ amesema.
Previous Post Next Post