Mwenyekiti wa halmashauri ya mji Kibaha,Mussa Ndomba,kulia akimkabidhi rasmi ufunguo wa shule hiyo Mkuu wa shule ya sekondari Koka,kushoto
Mchungaji wa Kanisa la FPCT akiongoza sala ya kuombea amani na baraka kwenye shule ya sekondari Koka
Na Daniel Limbe,Kibaha
KATIKA kukabiliana na mmomonyoko wa maadili kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari nchini, jamii imeaswa kushirikiana katika ulinzi na makuzi ya mtoto ili kujenga jamii yenye wasomi watakaosaidia mabadiliko ya sayansi na uchumi kwa jamii.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa halmashauri ya mji Kibaha,Mussa Ndomba,baada ya kushiriki maombi na dua kwenye shule ya sekondari Koka iliyopo kata ya Sofu wilayani Kibaha mkoani Pwani.
Katika maombi hayo yaliyolenga kuombea amani na baraka za Mwenyezi Mungu kwa walimu na wanafunzi wa shule hiyo kabla ya kuanza rasmi kwa masomo kwenye shule hiyo mpya, yameongozwa na viongozi mbalimbali wa dini wakiwemo mashekhe na wachungaji,viongozi wa vyama vya siasa,wananchi pamoja na wazee maarufu.
Hata hivyo katika kukabiliana na wimbi la utolo,uvutaji bangi na mimba za umri mdogo mashuleni,Ndomba akaitaka jamii kushirikiana kwa pamoja kudhibiti vitendo hivyo kwa wanafunzi waliosajiliwa kujiunga na shule ya sekondari Koka ili kuwa na wanafunzi bora kitabia na kielimu badala ya kuiachia serikali pekee.
Mkuu wa shule hiyo, Kharima Yusuph, mbali na kuipongeza serikali na jamii kwa kuanzisha shule hiyo,amedai mpaka sasa jumla ya wanafunzi 58 wamesajiliwa kuanza masomo pamoja na walimu 18 ambao watafundisha masomo yote ikiwemo somo jipya la kichina.
Ofisa elimu kata ya Sofu,Jane Tenga, amedai uwepo wa miundo mbinu bora ya kufundishia ikiwemo madarasa,walimu na wanafunzi hao, jamii itegemee kupata wasomi wazuri kutoka shule hiyo na kwamba wanafunzi hawatalazimika kutembea umbali mrefu kwenda shule ya sekondari nyumbu kama ilivyokuwa awali.
Kwa upande wake mtendaji wa Kata hiyo,Saumu Hassan, ameitaka jamii kuendelea kuchangia miradi ya maendeleo kwa lengo la kuongeza ustawi wa vijana ambao ni taifa la kesho,huku akiahidi kuendelea kushirikiana na jamii kuhakikisha kata ya sofu inafanikiwa kitimiza malengo iliyojiwekea.
Akiongea kwa niaba ya viongozi wenzake wa dini,Mchungaji wa Kanisa la Free Pentecost Church of Tanzania(FPCT) Mathayo Mbilizi, amesema njia bora ya kufanikiwa katika maendeleo yoyote duniani lazima Mwenyezi Mungu awe ndiyo kiongozi wa kwanza kutukuzwa,huku akiupongeza uongozi wa shule hiyo kuwa na maono ya kuwaalika viongozi wa dini kufanya maombi na dua kabla ya kuanza rasmi kwa masomo kwenye shule hiyo mpya.