Wafanyakazi wa Bank ya CRDB tawi la TAZARA, wakisiliza maelezo kuhusu kaya ya wazanaki, kutoka kwa Mhifadhi mwandamizi wa Kijiji cha Makumbusho Bw.Wilbard Lema. Waliweza kufurahia na kupongeza uhifadhi unaofanywa na Kijiji cha Makumbusho.
Bi. Jane John akiwa kwenye nyumba ya asili ya watu wa Kigoma (waha) mara baada ya kutembelea Kijiji cha Makumbusho.
Meneja wa huduma kwa wateja Bi. Rosalia Mlambili akitoke kwenye moja ya nyumba ya kabila la wagogo (Tembe), Nyuma yake ni Bi. Gema Shirima mara baada ya kutembelea Kijiji cha Makumbusho.
Na Mwandishi Wetu
Wafanyakazi wa Benki ya CRDB tawi la TAZARA wametembelea Kijiji cha Makumbusho na kufurahishwa na uhifadhi wa ujuzi wa ujenzi wa nyumba za asili za jamii mbalimbali ya Tanzania.
Wafanyakazi hao wakiongozwa na Meneja wa Tawi, Bw. Elishumbo Mwasha wametembelea Kituo hicho cha uhifadhi kama sehemu ya kuburudika na kujifunza juu ya mambo mbalimbali yanafanyika Kijiji hapo.
“Tumejifunza mambo mengi ambayo hatukujua kama yapo Kijiji cha Makumbusho ikiwemo teknolojia ya ujenzi wa nyumba za makabila mbalimbali ambapo kila mmoja wetu amefika na uona nyumba ya kijijini kwao.
Bw Mwasha amesema kuna haja ya Watanzania kuleta watoto wao katika Kijiji cha Makumbusho ili waweze kujifunza mambo mbalimbali ya mila na desturi za jamii zao.
“Nimefurahi sana kutembelea Kijiji cha Makumbusho nitawaleta watoto wangu wote waje kujifunza mila na desturi za kabila (Wachaga) yetu ikiwa ni pamoja na jinsi babu zetu walivyoishi” amesema Bw. Mwasha.
Meneja wa CRDB tawi la TAZARA ametoa wito kwa matawi mengne ya CRDB na taasisi zingine kutembelea Kijiji cha Makumbusho na vituo vingine vya Makumbusho ya Taifa ili waweze kujifunza mambo mbalimbali.
Naye Jane John alifurahia sana kuona nyumba ya kwao (Waha) na kusema kuwa imemkumbusha nyumbani kwao alikotokea Kigoma ambapo aliingia ndani ya nyumba hiyo na kukaa chini huku akidai apigwe picha ya kumbukumbu.
“Jamani nyumba hii imenikumbusha nyumbani kwetu Kigoma, nimefurahia sana uhifadhi huu” alisema Bi Jane.
Kila mmoja wao alijisikia vizuri alipoiona nyumba iliyowakilisha jamii yao na kutotamani kuondoka katika maeneo hayo na kuahidi kurudi tena ili kujifunza zaidi.
Kijiji cha Makumbusho kilianzishwa mwaka 1966 kwa lengo la kuhifadhi ujuzi wa ujenzi wa nyumba za asili za jamii Tanzania.
Kaimu Mkurugenzi wa Kijiji cha Makumbusho, Bw Wilbard Lema amesema nyumba hizo katika Kijiji cha Makumbusho zinajengwa kwa kwa mtindo wa kaya kwa kufuata ramani ya Tanzania na kwamba zinajengwa kwa kushirikiana na jamii husika.
Bw. Lema ametoa wito kwa Makabila mbalimbali nchini kujitokeza ili kujenga nyumba za makabila yao kwa kushirikiana na Makumbusho ya Taifa.