Serikali imepokea Euro milioni 6 sawa na shilingi bilioni 13.2 kutoka Shirika la Ujerumani la GTZ kwa ajili ya mradi wa kupunguza migogoro baina ya binadamu na wanyamapori hasa kwenye maeneo ya pembezoni mwa hifadhi.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Mary Masanja (Mb) wakati wa ziara ya kikazi katika Chuo cha Mafunzo ya Maliasili kwa Jamii Likuyu Sekamaganga Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma.
“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ametafuta fedha kiasi cha shilingi bilioni 13.2 ambazo zitatumika katika kufanya utafiti wa maeneo yenye changamoto za wanyama wakali na waharibifu, kutoa elimu kwa jamii zinazoishi pembezoni mwa hifadhi kuhusu uhifadhi na kukabiliana na wanyama wakali na waharibifu” Mhe. Masanja amesisitiza.
Amesema mradi huo wa miaka mitatu una lengo la kutoa ujuzi kwa jamii kuhusu namna ya kukabiliana na wanyama wakali na waharibifu ambapo jamii hizo zitasambaza ujuzi kwa jamii nyinginezo.
Aidha, amesema mafunzo hayo pia yatatolewa kwa Askari Wanyamapori wa Vijiji(VGS) ili kuongeza nguvu ya kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu.
Mhe. Masanja amefafanua kuwa endapo jamii zikipata uelewa wa namna ya kuhifadhi na kukabiliana na wanyama wakali na waharibifu hakutakuwa na chuki baina ya binadamu na shughuli za uhifadhi.
Naye, Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Maliasili kwa Jamii Likuyu Sekamaganga, Jane John amesema kuwa chuo hicho kinatoa mafunzo ya Askari wa Wanyamapori wa Vijiji, Askari wa Misitu wa Vijiji, Askari wanaosimamia fukwe za jamii, kozi kwa viongozi na wajumbe wa kamati za maliasili za vijiji, Astashahada ya Utalii na Waongoza Watalii pamoja na mafunzo ya kudhibiti wanyama wakali na waharibifu.