SERIKALI YAISHUKURU GAVI KWA MSAADA WA SHILINGI TRILIONI 1.3 ZA HUDUMA ZA CHANJO NCHINI



Na WAF – New York, Marekani.
 
Serikali kupitia Wizara ya Afya imeishukuru Shirika la GAVI kwa kuipatia Tanzania msaada wa shilingi trilioni 1.3 kuanzia mwaka 2000 kwa ajili ya huduma za chanjo na kuimarisha mifumo ya afya.

Shukrani hizo zimetolewa na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu alipokutana na Mtendaji Mkuu wa Shirika la Kimataifa linalojishughulisha na upatikanaji wa chanjo (GAVI) Dkt. ESeth Berkley wakati wa kikao cha pembezoni mwa Mkutano wa 77 wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa unaoendelea jijini New York, Marekani. 
 
“Tunaishukuru GAVI kwa kuipatia Tanzania msaada upatao shilingi trilioni 1.3 kuanzia mwaka 2000 kwa ajili huduma za chanjo na kuimarisha mifumo ya afya. Ufadhili huo umewezesha watoto walio chini ya miaka mitano kujikinga na magonjwa au vifo vitokanavyo na magonjwa kama Kifua Kikuu, Surua na Polio” amesema Waziri Ummy Mwalimu.
 


Aidha, Waziri Ummy alilipongeza Shirika hilo kwa kuwa mshirika mkuu wa Mpango wa COVAX ambao umewezesha uzalishaji na upatikanaji wa msaada wa chanjo ya UVIKO-19 katika nchi za kipato cha chini na kati. Hadi hivi sasa Tanzania imepata msaada wa chanjo zaidi ya milioni 20 ushiriki ili kuwakinga wananchi wake na UVIKO-19. 
 
Amesema kuwa tathmini iliyofanyika mwaka 2020/2021 imeonesha kushuka kwa kiwango cha uchanjaji  kwa watoto walio chini ya miaka mitano kwa asilimia tano nchini Tanzania kutoka asilimia 97 kwa mwaka 2018/2019. Hali hii imechangiwa na janga la UVIKO-19 ambapo msukumo mkubwa wa huduma za kinga uliwekwa katika uchanjaji wa chanjo ya UVIKO-19. Aidha, chanjo dhidi ya ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi imeshuka katika kipindi hicho. 
 
Hata hivyo Waziri Ummy amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya, imejipanga kuimarisha huduma hizo za chanjo kwa watoto walio chini ya miaka mitano na wasichana balehe ili kujikinga na magonjwa ya kuambukiza. 
 


“Serikali imeweka mikakati ya kuongeza wigo wa uchanjaji kama vile kutumia huduma mkoba na tembezi ili kufikia makundi ambayo hayajapata chanjo, kujumuisha huduma za chanjo kwenye huduma za chanjo na kufanya kampeni mahususi za kuongeza kiwango cha uchanjaji” Amesema Waziri Ummy Mwalimu.
 
Kwa upande wake Dkt Berkeley, alimfahamisha Waziri Ummy kuwa GAVI itaanza kusaidia upatikanaji wa chanjo baada ya kujiridhisha na utafiti uliofanyika nchini Kenya, Malawi na Ghana kuhusiana na chanjo dhidi ya ugonjwa wa Malaria kwa watoto chini ya miaka mitano. Hivyo shirika hilo litaanza kupokea maombi kutoka nchi zenye mzigo mkubwa wa ugonjwa huo mwaka 2023. 
 
Dkt Berkley ameahidi kuwa Shirika la GAVI litaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuongeza wigo wa uchanjaji kwa watoto chini ya miaka mitano na wasichana walio kwenye kundi balehe ili kujikinga na saratani ya mlango wa kizazi.


Previous Post Next Post