Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema hali ya uchapaji usambazaji wa vitabu vya ziada vyenye ithibati inaukakasi hivyo Serikali kuanzia mwakani itatenga bajeti ya Bilioni moja ili kunusuru kwa kununua vitabu na kuvipeleka mashuleni ili kuleta hamasa.
Ameyasema hayo leo katika Uzinduzi wa Tuzo ya Taifa Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu ambapo amesema kupitia tuzo hiyo wanafungua ukurasa wa kuchochea hari mpya ambapo mwakani serikali itatenga fedha ya kusimamia vitabu vya ithibati.
“Tumetenga kwenye bajeti kiasi cha shilingi bilioni moja kwa ajili ya kuhakikisha tunaanzia kutekeleza mapendekezo ya wadau wetu na taratibu zote zitafanyika chini ya TET lengo ni kukidhi matakwa ya wadau kuchangamsha soko siyo kushuhudia baadhi ya taasisi za uchapashaji zinafungwa “amesema Mkenda
Hata hivyo amesema Mwandishi atakayepata tuzo watahakikisha kitabu chake kinachapwa na kununua kisha kukisambaza kuanzia mashuleni hadi maktaba ya Taifa Ili kumsaidia kufidia gharama zake alizotumia.
Kwa upande wake Kamishna Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Lyabwene Mtahabwa amewasisitiza Waandishi wa vitabu kuandika kuhusu watoto kwani wamekuwa wakipitia changamoto ya mazingira magumu kwa kufanyiwa vitendo viovu ndani ya Jamii na wahusika ni ndugu zao wa karibu vitendo hivyo ni pamoja na kulawitiwa kubakwa,kupigwa,kunyanyapaliwa hivyo wakiandika vitabu itasaidia kubadilisha Jamii
“Watoto ni tunu kubwa tuliyopewa na Mwenyezi Mungu kuwa baraka lakini Leo tukiwaangalia baadhi ya watoto wanavyoteseka kutokana na changamoto wanazokutana nazo machozi yananitoka kila nikisoma magazeti visa na mikasa yao ni vya kutisha kalamu yenu itawaokoa”. Amesema Prof.Mtahabwa.
Naye Mwenyekiti Tuzo ya Taifa Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu Bi.Penina Mrama amesema Mbunifu atakayeshiriki atatakiwa kuandika nyanja moja tu kwa mada atakayoichagua yaani riwaya au ushairi na andiko liwe makini litakalojikita katika masuala ya kijamii na dirisha ya kuwasilisha kutakuwa wazi kuanzia Septemba 13- Novemba 30 mwaka huu.
Aidha amesema majaji watapitia maandiko ya kila mshiriki atakayetuma kupitia barua pepe na Zawadi nono Kwa washindi itakuwepo ambapo mshindi wa kwanza atapewa kiasi cha shilingi milioni 10 huku wa pili akipatiwa shilingi milioni 7 na watatu atapewa milioni 5 hivyo Waandishi wote wa vitabu andikeni kazi nzuri na hii itakuwa kila mwaka .