Na Daniel Limbe,Kibaha
JAMII imeaswa kwenda kupata huduma za tiba ya kichaa cha mbwa kwenye vituo vya kutolea huduma za Afya badala ya kwenda kwa waganga wa jadi, hali inayoweza kusababisha vifo visivyokuwa vya lazima.
Hayo yamebainishwa leo na Ofisa mifugo kata ya Sofu,Grory Amos,wakati akitoa elimu ya umuhimu wa chanjo ya mbwa kwa wakazi wa kata hiyo,huku akiwaonya kutokimbilia kwa waganga wa jadi kupata tiba ya kichaa cha mbwa.
Amedai kuwa kichaa cha mbwa hakina tiba na kwamba wanachokifanya ni kutoa chanjo ili kuwakinga na virusi vinavyosababisha ugonjwa huo hatari kwa jamii.
Sambamba na hilo amedai kwamba mtu anapoambukizwa ugonjwa wa kichaa cha mbwa hupaswa kupata tiba sahihi kwa kipindi cha miezi mitatu mfululizo.
"Ninapenda kuiasa jamii kutambua kuwa kichaa cha mbwa hakitibiwi kwa waganga wa jadi...ili mtu aliyeambukizwa aweze kupona anapaswa kuwahi kwenye Zahanati,kituo cha afya au hospitali zinazotambuliwa na serikali"amesema Amos.
Kwa upande wake Ofisa mtendaji wa mtaa wa sofu,Debora John,amesema ili kukabiliana na ugonjwa wa kichaa cha mbwa,jamii inapaswa kuendelea kupata elimu sahihi ya ufugaji wa mbwa badala ya kuendelea kufuga kwa mazoea.
Aidha amewataka wananchi kutoa taarifa haraka kwa viongozi wa mitaa na kata iwapo wataona mbwa mwenye dalili za ugonjwa wa kichaa cha mbwa kwa lengo la kunusuru jamii kukumbwa na maradhi hayo.
Naye Ofisa maendeleo ya jamii kata hiyo,Lilian Wilfred,ametumia fursa hiyo kuwaonya wananchi wote wanaofuga mbwa pasipo kuzingatia sheria,taratibu na kanuni za ufugaji na kwamba iwapo ikithibitika mbwa mwenye ugonjwa huo kusababisha madhara kwa jamii hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Leo ikiwa ni maadhimisho ya siku ya kichaa cha mbwa duniani, halmashauri ya Mji Kibaha yenye Mitaa 73 na Kata 14 inakadiriwa kuwa na Mbwa 3114 na Paka 930.