WIZARA YA MALIASILI NA UTALII KUENDELEA KUELIMISHA WANANCHI MBINU ZA KUKABILIANA NA TEMBO


Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii itaendelea kuelimisha wananchi kuhusu mbinu mbalimbali za kukabiliana wanyama wakali na waharibifu hususan tembo ili kupunguza madhara yatokanayo na wanyamapori hao.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) alipokua akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii kwenye kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kilichofanyika leo jijini Dodoma.



“Serikali ina mikakati ya kupunguza changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu kwa kuongeza idadi ya askari wa uhifadhi na kuwepo kwa namba maalum ambazo wananchi watapiga bure ili kutoa taarifa wanapovamiwa na wanyama wakali”Mhe. Masanja ameongeza.

Aidha, amesema Serikali ina mpango wa kuwafunga tembo viongozi vinasa mawimbi maalum (collar) ili kufuatilia muelekeo wa makundi ya tembo kwa lengo la kuwadhibiti pindi wanapoelekea katika makazi ya watu.


Amesema Wizara itaendelea kujenga mahusiano mazuri na Halmashauri za Wilaya ili kusaidiana kupunguza changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu hususan tembo.

Katika hatua nyingine, Mhe. Masanja amewaomba wabunge kuelimisha wananchi kutoendelea kuharibu maeneo ambayo ni mazuri kwa ajili ya kufugia nyuki ili kutokingana na sheria za uhifadhi.

Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhe. Juma Ally Makoa (Mb) ameitaka Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kuimarisha mbinu za kudhibiti tembo.


Pia ameiomba Wizara itoe elimu kwa Madiwani na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa kuhusu namna bora ya kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu hususan tembo.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Prof. Eliamani Sedoyeka ametoa rai kwa wabunge kuendelea kuwashawishi wananchi kutunza mazingira kwa kupanda miti ili kuhifadhi mazingira pia kutumia nishati mbadala.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi ,Maliasili na Utalii inaendelea na vikao kati yake na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa lengo la kujua utekelezaji wa shughuli na miradi mbalimbali ya Wizara hiyo.
Previous Post Next Post