Na Englibert Kayombo - Bungeni Dodoma.
Kamati ya kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii imeitaka Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) kufanya tafiti zenye kuleta majibu ya kutatua changamoto za afya zinazowakabili Watanzania ikiwemo Magonjwa yasiyoambukiza ambayo hivi karibuni yamekuwa yakiongezeka kwa kasi.
Hayo yamesemwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe Aloyce John Kamamba (Mbunge) leo kwenye kikao cha Kamati hiyo pamoja na Viongozi, na Watendaji wa Wizara pamoja na NIMR kilichofanyika katika kumbi za mikutano ya Bunge Jijini Dodoma.
“NIMR ni taasisi nyeti ya Serikali, ina wajibu mkubwa wa kulinda jamii yetu na kuja na majibu ya tafiti mbalimbali za magonjwa ili Jamii yetu iweze kupata majibu yatakayowasaidia kujikinga zaidi kuliko kusubiri kwenda kupata tiba” amesema Mhe. Kamamba.
Aidha Kamati imeishauri NIMR kuwekeza zaidi kwenye tafiti za dawa tiba asili na kuchunguza usalama wa dawa hizo kabla hazijafika kwa Jamii.
Kamati imeitaka NIMR kushirikiana kwa ukaribu zaidi na Msajili wa Tiba Asili ili katika kuchunguza usalama wa tiba asili hizo pamoja na kuongeza wazalishaji wengi wa tiba asili ambazo zitatumika na Jamii kwa ajili ya tiba mbalimbali.
Awali akizungumza Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema Serikali imekuwa ikitenga fedha za uendeshaji wa Taasisi hiyo na kuiwezesha kufanya tafiti mbalimbali zinazogusa maslahi ya moja kwa moja ya wananchi.
Waziri Ummy amesema kuwa NIMR ni taasisi kongwe na nyeti ya Serikali na imekuwa ikifanya tafiti mbalimbali hapa nchini kwa muda mrefu hivyo Serikali itaendelea kufanya maboresho zaidi ili kuiwezesha taasisi hiyo kufanya kazi kwa ufanisii zaidi.
Kwa upande wake Prof. Abel Makubi Katibu Mkuu Wizara ya Afya, amesema kuna ongezeko kubwa la magonjwa yasiyoambukiza nchini ambayo kwa wengi yanawapata kutokana na mtindo usio bora wa maisha na kutozingatia kufanya mazoezi.
Amesema Wizara inafanya mapitio ya Sera ya Afya ya Mwaka 2007 ili kuweza kuendana na hali iliyopo sasa katika kupambana na Magonjwa yasiyoambukiza na kuahidi kuwa Serikali itaendelea kuiwezesha NIMR kwa kutoa rasimali zitakazoiwezesha NIMR kufanya kazi zenye tija kwa Taifa.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu Prof. Yunus Mgaya amesema mwaka wa fedha ulioishia tarehe 30 Juni 2022, NIMR ilitekeleza miradi ya utafiti mikubwa, ya kati na midogo ipatayo 126 huku baadhi ya miradi ikiwa bado inaendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
“Miradi hii imelenga kutoa majibu na takwimu zinazohusu magonjwa ya kuambukiza na magonjwa yasiyoambukiza, uimarishaji wa mifumo ya afya, magonjwa ya milipuko na dharura, tiba asili, viashiria vya kijamii na kimazingira vya afya” amesema Prof. Mgaya
Prof. Mgaya amesema kuwa tafiti nyingi wanazofanya zimelenga katika kuboresha kinga, tiba na ufuatiliaji wa matibabu, tathmini za ubora wa tiba, vipimo vya maradhi ya kuambukiza na uimarishaji wa utoaji au upatikanaji wa tiba.