SERIKALI YATOA TAMKO TISHIO LA MGOMO WA MADEREVA



Serikali kupitia wizara ya Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu imetoa tamko kuhusu baadhi ya madereva wanaopotosha taarifa iliyotolewa na wizara hiyo juu ya posho zao na kuhamasisha madereva wenzao kugoma.

Taarifa iliyotolewa na Waziri wa wizara hiyo Profesa Joyce Ndalichako kwa waandishi wa Habari imesema kuwa, tarehe 22 Julai Serikali ilitoa taarifa kwa vyombo vya Habari kuhusu hatua zilizochukuliwa katika kushughulikia hoja na malalamiko yaliyowasilishwa na viongozi wa vyama vya wafanyakazi madereva na wamiliki wa vyombo vya usafirishaji nchini. 

Kufuatia kutolewa kwa taarifa hiyo, wapo baadhi ya Madereva ambao wameipokea kwa mtazamo tofauti.

Kutokana na hali hiyo, wamekuwa wakipotosha taarifa hiyo na kuchochea ama kuhamasisha Madereva wenzao kugoma.

 Uchochezi wa mgomo wao umejikita katika viwango vya posho ambavyo Madereva, Wamiliki wa Vyombo vya Usafiri na Serikeli waliafikiana katika vikao vya majadiliano. 

Viwango walivyokubaliana ni viwango vya chini vya posho za safari (Minimum allowances) ambapo waajiri hawaruhusiwi kulipa chini ya viwango hivyo.

 Kwa wale Waajiri ambao walikuwa wanalipa viwango ambavyo viko juu ya viwango vya chini vya posho za safari vilivyowekwa, hawaruhusiwi kushusha viwango hivyo kwani kufanya hivyo ni kosa kwa mujibu wa Sheria. 2 

Aidha Serikali kwa kutambua umuhimu wa sekta ya usafirishaji kwa uchumi wa nchi, inasisitiza kuwa nafasi ya majadiliano bado ipo wazi na hivyo Wafanyakazi Madereva ambao wana hoja na malalamiko zaidi ya yale yaliyofanyiwa kazi, wayawasilishe rasmi katika mamlaka zinazohusika ili yaweze kupatiwa ufumbuzi.  
Previous Post Next Post