Imeelezwa kwamba Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) ipo katika kampeni ya kuwawezesha wazalishaji wadogo wa mbolea nchini ili kuongeza kiwango cha uzalishaji na kukidhi mahitaji ya mbolea nchini ambapo kwa sasa ni asilimia kumi ya mahitaji ya mbolea inazalishwa nchini na kiasi kinachobaki kinatoka nje ya nchi.
Hayo yamebainishwa tarehe 15 Februari, 2022 na Kaimu Meneja wa Uzalishaji wa Ndani na Mazingira, Stephenson Ngoda alipokuwa akifungua mafunzo kwa wazalishaji wadogo yaliyofanyika mkoani Arusha yenye lengo la kuwajengea uwezo wa kimitaji na teknolojia rahisi kuwawezesha kuzalisha kwa tija.
Ngoda amebainisha kuwa agenda kubwa kitaifa ni kuongeza uzalishaji wa ndani wa mbolea ili kukidhi mahitaji ya wakulima na kukiri kuwa rasilimali kwa ajili ya uzalishaji wa mbolea nchini upo.
Amesema mafunzo hayo yana umuhimu mkubwa katika kuwawezesha wazalishaji wa ndani kuzalisha mbolea bora kwa tija ili kupunguza utegemezi wa viwanda vya nje ambapo kufuatia mlipuko wa Ugongwa wa Covid-19 bei ya mbolea imepanda na kusababisha changamoto kubwa kwa wakulima kuweza kumudu bei ya mbolea sokoni.
Akizungumza katika kikao hicho Afisa Mdhibiti Ubora Mkuu, Esther Kapakala amesema TFRA imeamua kufanya mafunzo hayo kanda ya Kaskazini kutokana na kuwa na wazalishaji wengi wa mbolea waliojikita katika uzalishaji wa mbolea za maji (Folier Fertilizer) pamoja na mbolea ngumu katika ukanda huo.
Amesema, wazalishaji wengi wamekuwa na changamoto za kuwa na miundombinu duni na mitaji hivyo kikao hicho kinawakutanisha wazalishaji hao na watoa huduma za kifedha ili kuwawezesha kupata mitaji na teknolojia bora itakayowawezesha kuzalisha kwa tija.
Kwa upande wake Meneja wa Mkoa wa Shirika la Viwanda Vidogo vodogo (SIDO) Nina Nchimbi amewataka wazalishaji wa mbolea kutafuta taarifa sahihi zinazohusiana na shughuli zao ili kuongeza tija katika uwekezaji wao na zaidi kupata ufumbuzi wa changamoto za mitaji zinazowakabili.
Amesema lengo kuu la shirika analolisimamia ni kuwasaidia wajasiriamali wadogowadogo kwa kuwapa ushauri katika uanzishaji wa viwanda na kuwarahisishia katika shughuli za usajili wa bidhaa wanazozalisha.
Amesema, kwa wajasiriamali wadogo ambao wamesimamiwa na kushauriwa na shirika hilo hupata urahisi wa bidhaa zao kukidhi viwango kutokana na ushauri fasaha wanaopewa na shirika hilo.
Pamoja na mwezeshaji kutoka SIDO, walikuwepo wawezeshaji kutoka NMB, CRDB, PASS, EFTA ambapo wote walieleza msaada wa kitaalamu wanaoutoa kwa wakulima ikiwa ni pamoja na uandishi wa maandiko ya biashara inayowawezesha kupata mikopo kwenye taasisi za kifedha, kuwakopesha vifaa au mitambo, na kuwapa ushauri wa kitaalamu katika uzalishaji wa mbolea ili kukidhi viwango vinavyokubalika kitaifa na kimataifa.



