Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amezindua Mpango Mkakati wa kudhibiti maambuzi ya Ugonjwa wa UVIKO-19 kwa Mkoa wa Dar es Salaam wenye lengo la kuthibiti kuenea kwa wimbi la nne la maambukizi hayo.
Dkt Gwajima amezindua Mpango huo Jiji Dar Es Salaam wakati wa Mkutano wa wadau wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwa Sekta ya Afya.
Dkt Gwajima amesema kuwa Serikali imeendelea kuwekeza katika Sekta ya Afya kwa kuhakikisha huduma za Afya zinaboreshwa kwa kujenga miundombinu mbalimbali na kuimarisha mifumo ya utoaji wa huduma za Afya.
Aidha,Dkt. Gwajima ameeleza kuwa Mkutano huo uliowakutanisha wadau hao wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini kwa Sekta ya Afya utasaidia kutatua changamoto zilizopo katika utoaji wa huduma za Afya na yatatoa majibu na muelekeo katika kuhakikisha huduma bora za Afya zinapatikana.
Akielezea kuhusu wimbi la nne la maambukizi ya Ugonjwa wa UVIKO-19 amesema Wadau hao wasaidia katika kutoa elimu kawa wananchi katika kuhakikisha wanazingatia ushauri wa wataalam wa afya katika kujikinga na maambukizi ya Ugonjwa huo.
Naye, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam Dkt. Rashid Mfaume ameeleza kuwa Mkoa umejipanga katika kuhakikisha unapambana na maambukizi ya Ugonjwa wa UVIKO-19 kwa wimbi la nne na hasa kuhakikisha utoaji wa huduma za Afya katika vituo vya Afya vilivyopo mkoani humo.
