Na Mwandishi wetu.....
Wananchi hususan wale walioko katika makundi yenye mahitaji maalumu wametakiwa kujitokeza kwa wingi kujisajili ili kupata Vitambulisho vya Taifa, hatua itakayorahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo afya, elimu na huduma za kifedha.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji Vitambulisho kutoka Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Bw. Edson Guyai, wakati wa zoezi maalum la usajili wa watu kutoka makundi maalumu, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Vitambulisho Duniani yaliyofikia kilele chake jijini Dar es Salaam.
"Tunaendelea na juhudi kuhakikisha kila Mtanzania anapata kitambulisho cha taifa ifikapo mwaka 2030, kama sehemu ya kutimiza malengo ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs). Makundi maalumu kama watu wenye ulemavu wanahitaji kipaumbele ili wasiachwe nyuma katika upatikanaji wa huduma," alisema Bw. Guyai.
Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii wa Manispaa ya Temeke, Bi. Ristituta Simon, alisema kuwa kumekuwa na mwitikio mdogo wa watu wenye ulemavu kujitokeza kupata huduma hiyo, hivyo zoezi hilo limekuwa msaada mkubwa katika kuwafikia walengwa.
“Changamoto kubwa imekuwa ni uelewa mdogo au ukosefu wa taarifa sahihi miongoni mwa baadhi ya watu wenye ulemavu. Kupitia kampeni hii, tumewaelimisha na kuwawezesha wengi kupata haki yao ya msingi,” alisema Bi. Ristituta.
Naye mmoja wa wananchi waliopata huduma hiyo, Bw. Maabadi Juma, alieleza kuwa kitambulisho cha taifa ni nyenzo muhimu katika maisha ya kila siku kwani kinahitajika kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali.
“Ni muhimu sana kwa wenzetu wenye mahitaji maalumu kujitokeza kwa wingi katika ofisi za NIDA. Kitambulisho hiki kinahitajika hata wakati wa kufungua akaunti benki au kupata huduma za matibabu,” alisema Maabadi