VIJANA WAHANDISI WATAKIWA KUTUMIA UBUNIFU KUTATUA CHANGAMOTO ZA TAIFA

 





Na Lilian Ekonga...


Katika hatua muhimu ya kuhamasisha ubunifu na uongozi miongoni mwa vijana wahandisi nchini, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Dkt. Charles Msonde, amewataka wahandisi vijana kuanza kuchukua hatua za kiuhandisi ambazo zitasaidia kuleta mabadiliko ya haraka katika sekta ya ujenzi na miundombinu nchini.


Akizungumza wakati wa kufunga Kongamano la Pili la Vijana Wahandisi (YEF) lililofanyika leo Septemba 24, 2025, Dkt. Msonde alisema kuwa vijana wahandisi wanapaswa kuwa mabalozi wa mabadiliko, kwa kutumia ubunifu wao kutatua changamoto za kiuchumi, kijamii, na kiteknolojia ambazo zinakumba taifa.


“Kama taifa, tunahitaji viongozi wa kiuhandisi ambao sio tu wanajua maarifa ya kitaalamu, bali pia wana uwezo wa kubuni suluhisho zinazozalisha ajira, kuongeza tija na kuboresha miundombinu yetu. Hatuwezi kufanikiwa kwa kuiga mifumo ya nje; ubunifu wetu na maarifa yetu ni suluhisho la changamoto zetu,” alisema Dkt. Msonde.


Pia, Dkt. Msonde alisisitiza umuhimu wa vijana wahandisi kushirikiana na sekta binafsi, serikali, na jamii katika kutoa suluhisho za kisasa za kimaendeleo ambazo zitaharakisha mageuzi ya taifa. Aliwahimiza wahandisi vijana kutambua kuwa wao ndio wenye uwezo wa kubeba majukumu ya kufanya mageuzi ya kitaifa kupitia ufanisi wa miradi ya uhandisi.



“Vijana wa leo ni viongozi wa kesho. Mnafursa ya kuwa mstari wa mbele katika kuleta mapinduzi ya kiuchumi na maendeleo ya kijamii. Huu ni wakati wenu, na dunia inawategemea,” aliongeza Dkt. Msonde.


Katika kongamano hilo, ambapo wahandisi vijana zaidi ya 140 walishiriki, Kaimu Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi Tanzania (ERB), Wakili Mercy Jilala, alieleza kuwa kongamano hilo lilikuwa na lengo la kuwajengea vijana uwezo wa kimaisha, ikiwemo kuwafundisha kuhusu namna ya kujiajiri, na siyo kutegemea ajira za serikali pekee.



“Vijana wahandisi wanapaswa kuwa na uwezo wa kubuni miradi ya uhandisi ambayo itawawezesha kuwa na nafasi katika soko la ajira, lakini pia kushiriki kikamilifu katika kuendeleza taifa. Huu ni wakati wa kujitokeza na kutoa mawazo mapya ambayo yataboresha mazingira ya kazi na maisha ya Watanzania,” alisema Wakili Jilala.


Kwa upande mwingine, Mwenyekiti wa Bodi ya ERB, Mhandisi Menye Manga, alisema kuwa kongamano hili limeonyesha kuwa vijana wahandisi wana uwezo mkubwa wa kuleta ubunifu na kwamba, bodi itaendelea kutoa fursa za mafunzo ili vijana waendelee kuwa na ujuzi unaohitajika katika soko la ajira linalobadilika kila siku.


“Vijana wanahitaji msaada katika kujua jinsi ya kuanzisha na kuendesha miradi ya uhandisi. Ni muhimu kuwa na mfumo wa mafunzo na makongamano kama haya ambayo yatakuza ubunifu na kuwezesha vijana kuchangia zaidi katika maendeleo ya taifa,” alifafanua Mhandisi Manga.


Kongamano hili, lilio na kauli mbiu "Mustakabali wa Uhandisi: Mageuzi ya Kitaifa Yanaongozwa na Suluhisho za Ubunifu za Vijana," limeweza kukutanisha wahandisi vijana pamoja na wataalamu wa sekta mbalimbali ili kubadilishana mawazo na kuzindua mipango inayoweza kubadilisha mustakabali wa uhandisi nchini.





Previous Post Next Post